Wanawake Pemba Watakiwa Kujiandaa Kushika Nafasi Za Uongozi Wa Juu.
Na Mwandishi Wetu Pemba.
Viongozi wanawake kisiwani Pemba wametakiwa kuyafanyia kazi mafunzo ya uongozi wanayopatiwa kwa kuandaa mikakati madhubuti itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kushika nafasi za juu za uongozi ifikapo 2030.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Jumuiya ya Mazingira jinsia na utetezi Pemba 'PEGAO' , Hafidh Abdi Said wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa madiwani na waratibu wa shehia wanawake, yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar ((TAMWA-ZNZ), Mkanjuni, Chake Chake, Pemba.
Amesema wanawake wanaotamani kufikia nafasi za juu za uongozi wanapaswa kuanza maandalizi mapema kwa kuyafanyia kazi maarifa wanayoyapata kupitia mafunzo mbalimbali, pamoja na kuwa na mipango kazi itakayowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
"Ni muhimu kwa viongozi wanawake kutambua kuwa nafasi za juu za uongozi zinahitaji maandalizi ya mapema. Hivyo, wanapaswa kuyafanyia kazi mafunzo wanayopatiwa, kujiwekea mipango madhubuti na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili wanapofika wakati wa kuwania nafasi hizo wawe tayari," alisema.
Alifafanua kuwa mafunzo hayo yanalenga pia kuonesha namna madiwani wanawake wanavyotekeleza majukumu yao na kukubalika katika jamii wanazoziongoza, jambo litakalosaidia kuongeza nafasi zao za kuaminiwa na kuchaguliwa kushika nafasi za juu za uongozi ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake, Afisa programu wa Mradi wa Kuwawezesha wanawake katika Uongozi kutoka chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar Sabrina Yussuf Mwantanga, alisema matarajio ya TAMWA-ZNZ ni kuona harakati za kuwaimarisha wanawake zikiendelea ili kupunguza mfumo dume unaoendelea kuwa kikwazo kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi.
Alifahamisha ni muhimu kwa wanawake waliopatiwa mafunzo hayo kuyatumia , kuongeza maarifa na kuimarisha uwezo wao wa kiuongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
"Matarajio yetu ni kuona wanawake wanazidi kuimarika katika uongozi, wanatumia maarifa wanayoyapata kuleta mabadiliko katika jamii na kujenga mazingira yatakayowawezesha wanawake wengi zaidi kujitokeza kuwania nafasi za uongozi ifikapo mwaka 2030," alisema.
Alieleza kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa juhudi za kuwajengea uwezo viongozi wanawake, huku yakitoa fursa ya kutathmini hatua walizofikia katika kutekeleza yale waliyojifunza kwenye mafunzo yaliyotangulia na kubaini changamoto wanazokabiliana nazo katika majukumu yao.
Akielezea namna mafunzo hayo yalivyomsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake, Diwani wa Wadi ya Mtambwe, Suhaila Omar Hamad, alisema yameimarisha ujasiri wake wa kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Alisema kupitia nafasi yake ameweza kushirikiana na mwakilishi wa jimbo lake la Mtambwe kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa huduma za maji katika Kijiji cha Kisiwani kwa Bint Abedi kwa kutoa shilingi laki tano kwa ajili ya usafishaji wa kisima pamoja na upatikanaji wa mipira ya maji.
"Baada ya kupata maarifa ya uongozi, nimekuwa na ujasiri zaidi wa kufuatilia changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi." alisema.
Aliongeza kuwa amewasaidia wanawake 70 kwa kuwapatia mtaji wa shilingi elfu 50,000 kila mmoja kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi, sambamba na kukabidhi mashine tano za fotokopi kwa skuli zilizomo ndani ya wadi yake.
Aidha, alisema ameshirikiana na Mwakilishi wa jimbo hilo kusaidia upatikanaji wa vikalio katika skuli za Tutu, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Katika kuendeleza ushiriki wa wanawake katika uongozi, alisema pia ameanzisha kikundi cha wanawake 30 kwa lengo la kuwapatia elimu na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Naye Diwani wa Wadi ya Michenzani, Mashavu Amour Mohd, alisema mafunzo hayo yamemsaidia kuhamasisha wanawake wengine kushiriki katika uongozi kwa kuwapatia elimu na kuwajengea uelewa kuhusu nafasi zao katika jamii.
"Baada ya mafunzo nimeweza kutoa elimu ya uongozi kwa wanawake 32 kutoka katika matawi sita yaliyomo ndani ya wadi yangu, sambamba na kuanzisha kikundi cha wanawake watano wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi," alisema.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na TAMWA Zanzibar ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa SWIL, unaolenga kuwajengea uwezo madiwani na waratibu wa shehia wanawake ili kuwaimarisha katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwaandaa kushiriki katika nafasi za juu za uongozi ifikapo mwaka 2030.



Wanawake ee, Wanawake Raaa
ReplyDelete