Breaking News

Baraza La Mji Kusini, Human Bridge Waridhishwa Na Matumizi Ya Vifaa Tiba Vilivyotolewa Katika Vituo Vya Afya


 Na Safian muhammed.

Upatikanaji wa vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha huduma za matibabu na kuokoa maisha ya wananchi, hususan akina mama na watoto.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Baraza la Mji Wilaya ya Kusini Unguja kwa kushirikiana na taasisi ya Human Bridge kutoka nchini Sweden, limefanya ziara maalumu ya kutembelea vituo vya afya vilivyonufaika na msaada wa vifaa tiba uliotolewa na taasisi hiyo, kwa lengo la kukagua matumizi ya vifaa hivyo na kutathmini mchango wake katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza katika majumuisho ya ziara hiyo, Daktari Mfawidhi wa Wilaya ya Kusini Unguja, Dk. Muhammad Mnyimbi, amesema vifaa tiba vilisambazwa katika vituo husika kwa kuzingatia mahitaji ya kila kituo ili kuhakikisha vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, hususan kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto.

Amesema hatua hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia vituo vya afya kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za matibabu.

Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kusini, Mussa Haji Mussa, pamoja na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Makame Ramadhani Makame, wamesema wataendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya afya katika wilaya hiyo.



Aidha, wamewahimiza wananchi kutumia ipasavyo vituo vya afya vilivyopo katika shehia zao ili kupata huduma za matibabu kwa wakati na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na kuchelewa kufuata huduma za afya.



Naye Mkurugenzi wa taasisi ya Human Bridge Tanzania, Bahati Kito, amesema ziara hiyo ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Baraza la Mji Kusini, pamoja na kujenga imani katika kuhakikisha misaada inayotolewa inawanufaisha wananchi.

Amesema taasisi hiyo imeridhishwa na namna vifaa tiba vilivyotolewa vinavyotumika katika vituo vilivyonufaika, jambo linaloonesha kuwa msaada huo unaendelea kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

Ziara hiyo imehusisha kutembelea Kituo cha Afya Kizimkazi Mkunguni, Kituo cha Mazoezi Tiba kwa Watoto wenye Changamoto za Kiafya kilichopo Makunduchi, Kituo cha Afya Bwejuu pamoja na Kituo cha Afya ya Mama na Mtoto kilichopo Paje.


No comments