WAZIRI AAGIZA MECCO KUENDELEZA UJENZI BAADA YA UFAFANUZI WA MIPAKA MUYUNI.
Na Said Khamis
Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Mhe. Shaaban Ali Othman, ameridhishwa na ufafanuzi uliotolewa na maafisa wa Kamisheni ya Ardhi kuhusu umiliki na mipaka ya eneo la Idara ya Maendeleo ya Vijana lililopo Muyuni, Wilaya ya Kusini Unguja, na ameielekeza Kampuni ya Mwananchi Engineering and Contracting Company (MECCO) kuendelea na shughuli za ujenzi.
Ufafanuzi huo umetolewa huko Baraza la Mji kusini wakati wa kikao cha Mashauriano kufuatia sintofahamu ya mipaka kati ya eneo la Idara ya Maendeleo ya Vijana na Ndugu Salum Ali Sleiman.
Amesema kuwa Kwa mujibu wa maofisa kutoka Kamisheni ya Ardhi, walieleza kwamba Idara ya Maendeleo ya Vijana inamiliki hati ya eneo hilo iliyotolewa mwaka 2009, huku Bwana Salum akipatiwa kitambulisho cha matumizi ya eka mwaka 2013.
Aidha wameeleza kuwa eneo linalodaiwa na Bwana Salum limeingia kimakosa kwa takribani asilimia 75 ndani ya eneo la Idara hiyo hali iliyosababisha sitofahamu ya kimipaka.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Othman Ali Maulid, ameagiza uhakiki wa wananchi wenye mashamba katika eneo hilo ili kuzuia kuongeza kwa changamoto ya mipaka.
Amesema uongozi wa Mkoa na Wilaya, kwa kushirikiana na Kamisheni ya Ardhi, utahakikisha unasimamia zoezi Hilo la kufanya uhakiki ili kila mwananchi anayestahiki kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Bwana Salum Ali Sleiman amesema hakuwa akifahamu awali kuhusu dosari hiyo na ameahidi kushirikiana na Serikali katika kuwaletea Maendeleo wananchi wake


No comments