Breaking News

WAZIRI ASISITIZA UMAKINI KATIKA UTOAJI WA MAAMUZI YA KESI ZA ARDHI.



 Na Said Khamis.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Rahma Kassim Ali, amewataka watendaji wa Mahakama ya Ardhi Zanzibar kuongeza umakini katika utoaji wa maamuzi ya kesi za ardhi zinazowasilishwa mahakamani hapo.

Akizungumza katika muendelezo wa ziara zake za kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara hiyo na kuzungumza na watendaji, huko katika ofisi za Mahakama ya Ardhi Mwanakwerekwe, Mhe. Rahma amesema taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa utoaji wa maamuzi ya kesi unazingatia umakini wa hali ya juu.

Amefafanua kuwa Mahakama ya Ardhi ni miongoni mwa taasisi muhimu zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja kupitia huduma zake, hivyo watendaji hawana budi kuwa waadilifu na kuharakisha kutoa maamuzi ya kesi za ardhi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Salha Mohammed Mwinjuma, amesisitiza umuhimu wa watendaji kuwa waadilifu katika kazi zao na kujiepusha na tamaa ili kuhakikisha haki inatendeka katika usuluhishi wa migogoro ya ardhi inayowasilishwa mahakamani hapo.



Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Khadija Khamis Rajab, amesema wizara tayari imekamilisha mchakato wa kuhamisha majukumu kutoka Mahakama ya Ardhi kwenda Mabara ya Ardhi. Ameeleza kuwa sheria iko kwa Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya hatua za mwisho, jambo litakalowezesha taasisi hiyo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mahakama hiyo, Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi, Fatma Muhajir Omar, amesema licha ya changamoto mbalimbali, taasisi hiyo imefanikiwa kutoa maamuzi ya mashauri 181, ambapo mashauri 113 yametolewa maamuzi kwa upande wa Unguja na mashauri 68 kwa upande wa Pemba.




No comments