ELIMU YA KUZUIA UDHALILISHAJI KUPUNGUZA MATUKIO KATIKA MASOKO YA SAMAKI NUNGWI.
Na Said Khamis.
wakati Dunia ikiwa katika siku 16 za kupambana na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia utolewaji wa elimu kuhusu udhalilishaji wa kijinsia katika masoko ya samaki na maeneo ya madiko ya wavuvi umeendelea kuleta mafanikio makubwa katika Shehia ya Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, huku watumiaji wa soko wakionesha uelewa mpana kuhusu athari za vitendo hivyo na namna ya kuviriripoti.
Katibu wa Uvuvi wa Shehia ya Nungwi, Bw. Khamis Hafidh Ali, amesema kuwa elimu wanayoitoa kwa wavuvi na wachuuzi imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya udhalilishaji. Aidha amewataka wanaofika sokoni kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kuendeleza utamaduni wa kuheshimiana.
“Mimi binafsi nilipewa mafunzo na Save the Children. Nimekuwa nikipitisha elimu hiyo kwa wenzangu kila tunapokaa kabla ya mnada. Hii imekuwa ikisaidia jamii yetu kubaki salama,” alisema Bw. Khamis.
Ameongeza kuwa mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali huwa wanapita mara kwa mara kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, ikiwemo kwa mtu mmoja mmoja sokoni. Hatua hii imeongeza mwamko na kupunguza lugha zisizofaa ambazo zamani zilikuwa zikichukuliwa kuwa sehemu ya utani wa masoko.
Ameeleza kuwa udhalilishaji si lazima uwe wa kimwili; hata kutoa maneno ya matusi au dharau ni aina ya udhalilishaji. “Tunashukuru kwamba tabia ya kutoleana maneno ya matusi katika soko letu imepungua sana kutokana na elimu tunayoendelea kuitoa,” aliongeza.
WATUMIAJI WA SOKO WATOA MAONI YAO
Kadhalika, watumiaji wa soko la Nungwi wakiwemo wanunuzi na wananchi wanaofika kwa shughuli mbalimbali wamepongeza juhudi za utoaji wa elimu na kubainisha kuwa sasa wana uelewa mkubwa kuhusu namna udhalilishaji unavyojitokeza.
WAVUVI NA WACHUUZI WAAPA KUENDELEZA MAPAMBANO
Kwa upande wao, wavuvi na wachuuzi wameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa shehia kuhakikisha wanaendelea kupokea na kusambaza elimu wanayopewa.
“Tabia ya kulindana ndiyo imekuwa ikisababisha vitendo hivi kuzidi. Sasa tumeamua kuwa tukiona mtu anakiuka maadili, tutaripoti bila kuangalia ukaribu,” walisemawavuvi hao.
Wamesema wanaamini kuwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kutasaidia Shehia ya Nungwi na hata maeneo mengine kubaki salama na kuepusha vitendo vya udhalilishaji, hasa kwa wanawake na watoto.
Uelewa huu mpana wa watumiaji wa soko, sambamba na juhudi za viongozi na mashirika, umeifanya Nungwi kuwa mfano wa maeneo yanayopiga hatua katika mapambano dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia hususan katika kipindi hiki cha siku 16 za kupambana na ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Reviewed by ZANNEWS UPDATE
on
November 28, 2025
Rating: 5



No comments