Breaking News

ATHARI KUBWA ZA UKATAJI MITI ZABAINIKA DUNIANI: WANANCHI WATAKIWA KUHAMIA NISHATI SAFI KUOKOA MAZINGIRA.

 


Na Said Khamis

Wananchi pamoja na taasisi za serikali na binafsi wametakiwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kuhamia kwenye nishati mbadala, ili kuzuia uharibifu unaoendelea kuongezeka katika mfumo wa mazingira. 

Wito huu umetolewa wakati ambapo dunia inakabiliwa na athari kubwa za ukataji miti, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa misitu, kupotea kwa viumbe hai, na ongezeko la gesi chafu.

Afisa Mazingira kutoka Idara ya Mazingira Zanzibar, Sabri Indrisa Muslim, ameiambia IKHUAN MEDIA  kuwa serikali imeweka sera maalum ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa kuimarisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

“Sera imeweka mikakati maalum ikiwemo kushawishi makampuni ya gesi kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kufanikisha matumizi ya nishati mbadala. Lengo ni kuachana kabisa na kuni na mkaa, kwani hali hii inaharibu mazingira kwa kiwango kikubwa,” alisema Afisa Sabri.

Amesema kuwa vikao mbalimbali vimekuwa vikiendelea kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa mazingira ili kuongeza uelewa juu ya madhara ya kuendelea kutegemea kuni na mkaa ambavyo ndio chanzo kikubwa cha ukataji miti ovyo nchini.



ATHARI ZA UKATAJI MITI: TAKWIMU ZA KIMATAIFA ZATOA TASWIRA HALISI.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ya mwaka 2024, dunia inapoteza takribani hektari milioni 10 za misitu kila mwaka, hasa kutokana na ukataji miti kwa ajili ya kuni, mkaa, kilimo na uchomaji moto. Utafiti huo unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya kaya barani Afrika hutegemea kuni na mkaa kwa kupikia, hali inayoathiri kwa kiasi kikubwa misitu ya eneo hilo. aidha ripoti hiyo inaonesha kuwa Ukataji miti unachangia asilimia 20 ya hewa ukaa (carbon emissions) duniani, ambayo inaharakisha ongezeko la joto duniani.

kwa upande mwengine ripoti hiyo imeonesha kuwa Kupotea kwa misitu kumesababisha kuongezeka kwa mafuriko, mmomonyoko wa ardhi, na kupungua kwa mvua za msimu katika maeneo mengi ya tropiki, ikiwemo Afrika Mashariki.

Ripoti nyingine ya World Resources Institute (WRI) inaonyesha kuwa ukataji miti umeathiri zaidi ya asilimia 30 ya spishi za wanyama wanaoishi misituni, wengi wao wakiwa hatarini kutoweka.

Katika muktadha wa Zanzibar, pamoja na kuwa na sehemu ndogo ya misitu, takwimu zinaonesha kuwa maeneo ya vijijini yamekuwa yakipungua kwa kasi kutokana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa, jambo linalohatarisha mfumo wa ikolojia katika visiwa.



WANANCHIWANATOA MAONI.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na IKHUAN MEDIA nyakati tofauti  wamesema kwamba ukataji miti ovyo umesababisha kupungua kwa uwoto wa asili na kuongezeka kwa ukame katika maeneo mengi nchini.

“Tunajua watu wengi vijijini tumezoea kupika kwa kuni na wengine mkaa, lakini athari tunazoziona sasa zinatulazimisha kubadilika. Mabadiliko ya tabianchi yanatuathiri moja kwa moja,” walisema wananchi hao akiwemo Hemed Rashid mkaazi wa Kisauni na Amina Salum mkaazi wa Darajabovu.

Walisema hali ya misitu kupotea imeongeza kasi ya mmomonyoko wa ardhi kwenye mashamba na kupunguza uzalishaji wa mazao, jambo ambalo linaathiri moja kwa moja usalama wa chakula.

aidha wananchi hao wameiomba idara ya misitu kuwa na hatua kali zaidi kwa wale wanaohusika na ukataji miti kwa makusudi, kwani vitendo hivyo vinahatarisha mustakabali wa “Zanzibar ya kijani” na kuathiri vizazi vijavyo.



“Hatuwezi kuendelea kuona watu wanakata miti ovyo bila hatua. Lazima sheria zitumike ipasavyo,” walisema.

Kwa kuzingatia ripoti za kimataifa na hali inayoonekana ndani ya jamii, matumizi ya kuni na mkaa yana athari kubwa kwa mazingira, afya na uchumi.

Katika ulimwengu unaokumbwa na mabadiliko ya tabianchi, hatua ndogo kama kuacha kutumia mkaa na kuni zinaweza kuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika kulinda dunia na mazingira ya Zanzibar kwa vizazi vijavyo.


No comments