Breaking News

TAMWA- ZNZ Yazindua Tuzo za Uwandishi wa Habari 2026/2027.



Na Safia Mohammed

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimezindua rasmi tuzo za uandishi wa habari zinazozingatia usawa wa kijinsia kwa msimu wa mwaka 2026/2027, kwa lengo la kuhamasisha wanahabari kuibua changamoto, mafanikio na masuala yenye maslahi kwa wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na makundi mengine katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Tunguu, Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ, Nairat Abdalla Ali, alisema tuzo hizo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uandishi wa habari wenye ubora, unaotumia ushahidi na takwimu sahihi katika kuibua masuala yanayohitaji kupewa kipaumbele katika jamii.

Alisema tuzo hizo zinaingia msimu wa sita tangu kuanzishwa kwake, zikiwa na kaulimbiu isemayo “Kalamu Yangu, Mchango Wangu kwa Wanawake,” inayowataka waandishi kutambua nafasi na wajibu wao katika kutumia taaluma ya habari kuleta mabadiliko chanya na kuchochea maendeleo ya jamii.

Alifafanua kuwa kwa takribani miaka mitano, tuzo hizo zilikuwa zikiendeshwa kupitia Mradi wa Kuimarisha Uongozi wa Wanawake na Demokrasia (SWIL), kwa ushirikiano na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, lakini chama kimeamua kuziendeleza ili ziwe jukwaa endelevu la kuthamini mchango wa wanahabari.

Alisema kuendelezwa kwa tuzo hizo kunalenga kuhakikisha masuala ya usawa wa kijinsia yanaendelea kupewa nafasi katika vyombo vya habari, huku waandishi wakihamasishwa kufanya kazi zinazotoa mwanga kuhusu haki, changamoto na fursa zinazowakabili makundi mbalimbali ya kijamii.

Mkurugenzi huyo, alisema msimu wa mwaka huu utakuwa na makundi sita ya mashindano, ambayo ni uongozi wa wanawake, elimu, ukatili wa kijinsia, haki na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu, uhuru wa kujieleza pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema makundi hayo yamechaguliwa kwa kuzingatia umuhimu wake katika maendeleo ya jamii, yakilenga kuwapa waandishi fursa ya kuchunguza na kuandika kwa kina kuhusu changamoto, mafanikio na fursa zinazojitokeza katika maeneo hayo.

Aidha, Nairat alisema kazi zitakazoshindanishwa zinapaswa kuwa zimechapishwa katika vyombo vya habari au kurushwa hewani kuanzia mwaka 2026 hadi Machi 30, 2027, huku mashindano hayo yakiwa wazi kwa waandishi wote wa habari bila kujali ushiriki wao katika miradi maalumu.

Alisisitiza kuwa kazi zitakazowasilishwa zinapaswa kuonesha ubora wa uandishi, ubunifu, matumizi sahihi ya takwimu na ushahidi unaothibitisha taarifa zinazotolewa, huku vipindi vya redio na televisheni vikitakiwa kutokuwa na urefu unaozidi dakika 30.

Alieleza kuwa kila kundi litakuwa na washindi watatu, hivyo kufanya jumla ya waandishi 18 kupata nafasi ya kutambuliwa na kuthaminiwa kwa kazi zao zinazochangia kukuza uandishi wa habari unaozingatia usawa wa kijinsia.

Aliwataka waandishi wenye nia ya kushiriki kuwasilisha kazi zao katika ofisi za TAMWA-ZNZ zilizopo Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, au katika ofisi ya chama hicho Pemba, pamoja na kutumia barua pepe ya chama hicho kwa ajili ya kutuma kazi zao.

Aliongeza kuwa waandishi wanapaswa kutumia fursa hiyo kuibua masuala yenye maslahi mapana kwa wananchi, kutoa nafasi kwa sauti za wanawake na makundi yaliyo pembezoni, pamoja na kuandika habari zinazochochea uwajibikaji, usawa na maendeleo.

Kwa upande wake, Ofisa Miradi wa TAMWA-ZNZ, Khairat Haji, aliwataka wanahabari kuimarisha uandishi wa habari zinazohusu elimu, mabadiliko ya tabianchi na udhalilishaji kwa kufanya uchunguzi wa kina na kufuatilia taarifa ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi.

Alisema suala la elimu limepewa msisitizo zaidi katika msimu huu ikilinganishwa na msimu uliopita, ambapo Wizara ya Elimu itashirikishwa katika kuangalia hali halisi ya miundombinu ya skuli pamoja na mifumo na taratibu zinazosimamia sekta hiyo.

Khairat alieleza kuwa msisitizo huo unatokana na umuhimu wa vyombo vya habari kuchunguza changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, badala ya kuripoti matukio pekee, ili kutoa taarifa zinazoweza kusaidia kubaini mapungufu na kuhimiza hatua za kuboresha huduma za elimu.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, alisema uchambuzi uliofanyika mwaka 2024 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali uliangazia uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na masuala ya kijinsia, kwa lengo la kuwahamasisha waandishi kuandika kuhusu nafasi, changamoto na mchango wa wanawake katika kukabiliana na athari zake.

Aliongeza kuwa wanawake wana nafasi muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni muhimu kazi za habari kuonesha namna wanavyoathirika, hatua wanazochukua na mchango wao katika kutafuta suluhisho la changamoto hizo.

Akizungumzia suala la udhalilishaji, Khairat alisisitiza kuwa waandishi hawapaswi kuishia kuripoti tukio linapotokea, bali wanapaswa kufanya ufuatiliaji wa kina ili kubaini hatua zilizochukuliwa na mamlaka husika, mwenendo wa kesi na matokeo yaliyopatikana.

Alisema matumizi ya takwimu sahihi na taarifa zilizothibitishwa ni muhimu katika kuimarisha uaminifu wa habari, kuongeza uzito wa taarifa zinazowasilishwa kwa umma na kusaidia jamii kuelewa ukubwa wa changamoto zinazojadiliwa.

Alisisitiza kuwa kupitia tuzo hizo, TAMWA-ZNZ inalenga kujenga utamaduni wa uandishi wa habari unaokwenda zaidi ya kuripoti matukio, kwa kuhamasisha uchunguzi, uwajibikaji na utoaji wa taarifa zinazoweza kuchochea mabadiliko chanya katika jamii.


No comments