Masheha kaskazini Pemba Waaswa uwadilifu na Weledi.
Na Mwandishi Wetu, Kaskazini Pemba
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya, amewataka masheha walioteuliwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, akisisitiza kuwa uongozi bora unaanzia katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mgeni ametoa wito huo wakati wa hafla ya kuwaapisha masheha hao, ambapo amewataka kuweka kipaumbele katika kuzuia migogoro ya ardhi, kusimamia amani na utulivu pamoja na kuwashirikisha wananchi katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya jamii.
Amesisitiza kuwa masheha wana nafasi muhimu katika kuimarisha utawala bora kwa kuwa wao ndio viongozi waliopo karibu zaidi na wananchi katika ngazi za shehia.
Mapema, Afisa Mdhamini wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Thabit Abdalla Othman, pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salum Khamis, wamewataka masheha hao kuhakikisha usalama wa wananchi unaimarika katika maeneo yao.
Viongozi hao wameeleza umuhimu wa masheha kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi katika kulinda amani na utulivu.
Kwa upande wao, Wakuu wa Wilaya za Wete na Micheweni, Abdalla Rashidi Ali na Khatib Juma Mjaja, wamewataka masheha kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Wamesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha mahusiano kati ya viongozi na wananchi pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma katika ngazi za shehia.
Nao baadhi ya masheha walioapishwa, akiwemo Juwaria Khamis Makame wa Shehia ya Msuka Mashariki na Khamis Faki Simai wa Shehia ya Kizimbani, wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi wengine katika kuhakikisha amani, utulivu na maendeleo yanapatikana katika maeneo yao.
Uteuzi na uapisho wa masheha hao unatarajiwa kuimarisha utawala bora katika ngazi za shehia, kuongeza uwajibikaji wa viongozi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

No comments