Wanawake Wataka mabadiliko Sheria za Uchaguzi kuongeza ushiriki Wao 2030.
Na Abdul Sakaza.
Wanawake nchini wameitaka Serikali na wadau wa uchaguzi kufanya marekebisho ya sheria na mifumo ya usimamizi wa uchaguzi ili kuhakikisha kunakuwepo uwazi, haki na usawa katika michakato ya uchaguzi, hatua itakayoongeza fursa kwa wanawake kushiriki na kushika nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030.
Wito huo umetolewa katika mkutano wa kutathmini mafanikio na changamoto zilizowakabili wanawake wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, uliojadili pia namna ya kuboresha mifumo ya uchaguzi kwa kuzingatia maoni ya vyama vya siasa, Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi na wadau wengine.
Washiriki wa mkutano huo wamesisitiza umuhimu wa kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka 2025, ili kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kuimarisha demokrasia na kujenga mazingira rafiki kwa wanawake kushiriki katika siasa bila vikwazo.
Naibu Katibu wa Haki za Binadamu wa ACT Wazalendo, Mpavu Abdalla, amesema baadhi ya sheria na taratibu za uchaguzi zinahitaji kupitiwa upya ili kuimarisha usimamizi wa uchaguzi na kuhakikisha malalamiko yanayowasilishwa na vyama vya siasa pamoja na wagombea yanashughulikiwa kwa haki kwa kuzingatia sheria.
Amesema pia kuna haja ya kuangalia vikwazo vinavyowakabili wanawake wanaotaka kugombea nafasi za uongozi, hususan wale wanaotoka katika utumishi wa umma, ili kuhakikisha wanapata fursa sawa za kushiriki katika ushindani wa kisiasa.
Kwa upande wake, Chum Saleh Mohamed wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), amesema kushiriki kwake kwa mara ya kwanza katika uchaguzi na kugombea nafasi ya ubunge kumempa uzoefu muhimu wa kisiasa, huku akipata uungwaji mkono kutoka kwa chama chake na wananchi.
Amesema ushirikiano na pongezi alizopata kutoka kwa watu aliowahi kusoma, kucheza na kufanya kazi nao, wakiwemo watu wa koo na vyama vingine, vimempa hamasa ya kuendelea na safari yake ya kisiasa licha ya changamoto zinazoweza kuwakabili wagombea wapya.
Akizungumzia umuhimu wa mshikamano wa wanawake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Asha Abdi Makame, amewataka wanawake kuendelea kuungana, kuhamasishana na kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza uwakilishi wao katika vyombo vya maamuzi.
Amesema uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi ni muhimu katika kuhakikisha mahitaji, changamoto na vipaumbele vyao vinazingatiwa katika mipango na sera za maendeleo.
Ameeleza kuwa TAMWA-ZNZ imekuwa ikifanya juhudi za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi kupitia vipindi mbalimbali vya uchaguzi kuanzia mwaka 2010 hadi 2025, ingawa bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili wanawake wengi zaidi wapate nafasi za kugombea na kuchaguliwa.
Naye Mratibu wa Mradi wa Kuwawezesha Wanawake katika Uongozi na Demokrasia (SWIL), Sabrina Yussuf Mwintanga, amesema wanawake wanahitaji kuimarisha mshikamano na ushiriki wao ndani ya vyama vya siasa ili kuongeza nafasi zao za kupata uongozi.
Amesema changamoto za kiuchumi, hususan upatikanaji wa fedha za kuendesha shughuli za kisiasa, bado ni miongoni mwa vikwazo vinavyowakabili wanawake, hivyo kuna haja ya wadau mbalimbali kushirikiana kutafuta njia za kuwawezesha kiuchumi na kisiasa.
Ameongeza kuwa uzoefu wa wanawake waliofanikiwa kupata nafasi za uongozi, wakiwemo wa viti maalumu, unaonesha umuhimu wa mshikamano katika kusukuma mbele masuala ya maendeleo na uwakilishi wa wanawake.
Kwa upande wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Mkuu wa Divisheni ya Mipango, Lutfia Faida Haji, amesema tume imekuwa ikiunda kamati mbalimbali, ikiwemo Kamati ya Maadili ya Uchaguzi, kwa kushirikisha vyama vya siasa katika kusimamia maadili, amani na utulivu wakati wa uchaguzi.
Amesema tume hiyo imeendelea kukutana na wadau mbalimbali ili kusikiliza maoni yao na kujadili hatua za kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kisiasa, ikiwemo kuwahamasisha kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Jeshi la Polisi, Kamisheni ya Polisi Zanzibar, Omar Hassan, amewashukuru wananchi kwa ushirikiano walioutoa kwa jeshi hilo kabla, wakati na baada ya uchaguzi, akisema hatua hiyo ilisaidia kudumisha amani na usalama.
Amesema malalamiko yaliyowasilishwa kwa jeshi hilo yalipokelewa na kushughulikiwa, huku akihimiza kuendelezwa kwa ushirikiano kati ya wananchi, viongozi na vyombo vya dola katika kukabiliana na rushwa na ubadhirifu.
Kwa ujumla, maoni yaliyotolewa katika mkutano huo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya wanawake, vyama vya siasa, Tume ya Uchaguzi na vyombo vya dola katika kuondoa vikwazo vinavyozuia ushiriki sawa wa wanawake katika siasa.
Huku Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030 ukitarajiwa kuwa hatua nyingine muhimu katika safari ya demokrasia nchini, wadau wameeleza umuhimu wa kuanza mapema kufanya maboresho ya kisheria, kiuchumi na kimfumo yatakayowezesha wanawake wengi zaidi kushiriki katika kugombea na kushika nafasi za maamuzi.


.jpeg)

Wanawake tunawezaaaa, wanawake jasiri
ReplyDelete