Breaking News

Zanzibar na Oman Kuendelea Kuimarisha Ushirikiano wa Kidiplomasia na Kihabari

 

NA  SAFIA MOHAMMED

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo tayari kushirikiana na wanahabari wa Oman katika kuandaa maudhui  yanayolenga   kuimarisha  diplomasia  ya habari, utamaduni na utalii,  na kukuza ushirikiano kati  ya Zanzibar na Oman.

 Waziri Dkt. Riziki Pembe Juma, ameyasema hayo  katika kongamano la Jukwaa la waandishi wa Habari wa Oman  na Zanzibar.

Amesema, ushirikiano huo  utahusisha utayarishaji wa vipindi maalumu vya utamaduni vitakavyorushwa kupitia vyombo vya habari vya Zanzibar na Oman, ikiwemo televisheni na redio.

Sambamba na hayo amesema maudhui hayo yatasaidia kuonesha historia, utamaduni, urithi na fursa za utalii zilizopo katika pande hizo mbili, ambapo amewataka wanahabari kutumia nafasi hiyo kuandika habari zinazojenga uelewa na kuimarisha mahusiano ya watu wa Zanzibar na Oman.

Aidha Dkt. Riziki amewasisitiza waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma, kufanya uchunguzi na kuhakiki taarifa kabla ya kuzisambaza.

Kwa upande wake, Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar, Said bin Salim Al Sinawi, amesema mkutano huo ni fursa ya kuimarisha ushirikiano wa vyombo vya habari na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu historia na maisha ya watu wa Zanzibar na Oman.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Oman, Dkt. Mohammed bin Mubarak Al Araimi, amesema wanahabari wana nafasi kubwa katika kuhifadhi historia na kujenga daraja kati ya jamii hizo mbili, huku akipendekeza kuwepo kwa mafunzo ya pamoja, kubadilishana uzoefu na kuandaa habari za pamoja.

 Mwenyekiti wa Zanzibar Press Club, Abdalla Mfaume, amesema ushirikiano huo unapaswa kuwa wa muda mrefu na kuhusisha mafunzo, tafiti, warsha na miradi ya pamoja ya habari, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vinaweza pia kukuza utalii, utamaduni, biashara na uwekezaji kati ya Zanzibar na Oman.

Aidha  kongamano hilo, limetoa fursa kwa  waandishi wa habari wa Zanzibar kusaini makubaliano maalum ya mashirikiano kati ya waandishi wa habari wa Zanzibar na  Oman na kuahidi kuendelea ushirikiano.


No comments