Breaking News

Jamii Yaaswa Kutafuta na Kuhifadhi Hati Miliki za Ardhi na Mali

 NA SITI ALI.

Jamii imetakiwa kuhakikisha inatafuta na kuhifadhi hati miliki za ardhi na mali wanazomiliki ili kujiepusha na migogoro ya umiliki pamoja na changamoto za mirathi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (ZU), Dk. Sikujua Omar Hamdan, ameyasema hayo wakati akitoa elimu ya sheria kwa wananchi wa Shehia ya Bambi, ambapo alisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuwa na nyaraka halali zinazothibitisha umiliki wa mali.

Alisema kutokuwepo kwa nyaraka sahihi za umiliki wa ardhi na mali ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia migogoro ndani ya familia na jamii, hasa pale inapofika wakati wa kugawa mali kwa warithi.

Dk. Sikujua alisema suala la mirathi limekuwa likikabiliwa na changamoto kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu taratibu na sheria zinazohusika katika ugawaji wa mali za marehemu.

Alifahamisha kuwa baadhi ya familia huingia katika migogoro ya muda mrefu na kukata udugu baada ya kifo cha ndugu yao kutokana na kutokuwepo kwa makubaliano au taarifa sahihi kuhusu mali alizoacha marehemu.

Alisema hali hiyo inaweza kuepukwa iwapo wananchi wataweka kumbukumbu sahihi za mali zao na kuhakikisha umiliki wake unatambulika kisheria, ili kurahisisha mchakato wa mirathi pale inapohitajika.

Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Sikujua alisisitiza wananchi kutokubali kununua au kuhamisha umiliki wa ardhi na mali bila kufuata taratibu za kisheria na kuhakikisha wanapata nyaraka zinazotambulika.

Kwa upande wake, Ofisa Sheria kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) Aisha Maulid Khamis alisisitiza umuhimu wa jamii kupata elimu ya sheria mapema ili iweze kutambua haki na wajibu wake katika masuala ya ardhi, mirathi na mali.

Alisema uelewa mdogo wa sheria unaweza kuwafanya wananchi kufanya maamuzi ambayo baadaye huleta migogoro, hivyo akawataka kutumia huduma za kisheria pale wanapokabiliwa na masuala yanayohitaji ufafanuzi.

Naye Ofisa Ustawi kutoka ZU, Nassor Haji Juma, alisema wazazi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wao wanakuwa katika mazingira salama na wanapatiwa uangalizi unaostahili.

Alisema ulinzi wa watoto unahitaji ushirikiano wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi kutimiza wajibu wao katika malezi na ustawi wa watoto.

Katika kikao hicho, washiriki walisisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kupata elimu kuhusu mirathi na sheria za umiliki wa mali ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza ndani ya familia baada ya kifo cha mmoja wa wanafamilia.

Walieleza kuwa wananchi wanapaswa pia kuwa na utamaduni wa kuandika na kuhifadhi kumbukumbu za madeni wanayodai au wanayodaiwa, pamoja na kuweka wazi makubaliano ya kifedha baina ya wahusika.

Walisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa malalamiko na migogoro isiyo ya lazima, huku wakitoa wito kwa jamii kutumia njia za kisheria katika kushughulikia migogoro ya ardhi, mirathi na mali badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuongeza migogoro.

No comments