TAMWA Zanzibar Yaitaka Polisi Kuharakisha Uchunguzi wa Kifo cha Mwanafunzi Raiyan
NA ABDUL SAKAZA.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), kimeitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kuharakisha na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kifo cha Raiyan Hemed Amour, mwenye umri wa miaka 15, mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Skuli ya Sekondari Kizimbani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
TAMWA-ZNZ imesema mwili wa Raiyan
ulidaiwa kukutwa katika kichaka ukiwa na jeraha katika kiganja cha mkono wa
kulia, hali ambayo imeibua maswali kuhusu mazingira ya kutoweka kwake na
hatimaye kifo chake.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la
Polisi iliyotolewa Oktoba 5, 2026, Raiyan aliondoka nyumbani kwao katika Kijiji
cha Kwale Mpona, siku ya Ijumaa Oktoba 2, 2026, majira ya saa 12:00 asubuhi kwa
ajili ya kwenda skuli, lakini baadaye mwili wake ulionekana katika kichaka
akiwa amefariki dunia.
Katika tamko lake, TAMWA-ZNZ
imelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa haraka, wa kina na wa haki ili
kubaini mazingira ya kutoweka kwa mwanafunzi huyo, chanzo cha kifo chake pamoja
na kuwabaini watu waliohusika, endapo watapatikana, na kuwachukulia hatua kwa
mujibu wa sheria.
TAMWA-ZNZ imesema hatua madhubuti
dhidi ya wahusika ni muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka kwa marehemu na
familia yake, sambamba na kujenga imani ya wananchi katika mifumo ya haki na
ulinzi wa watoto.
Chama hicho pia kimesisitiza kuwa
Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakifanya juhudi mbalimbali
katika kuimarisha haki na ulinzi wa wanawake na watoto, ikiwemo kuhakikisha
watoto wa kike wanapata fursa sawa za elimu, ulinzi na kushiriki katika
maendeleo ya jamii.
Aidha, TAMWA-ZNZ imeitaka Serikali
kupitia mamlaka husika kuimarisha usalama wa watoto wanapokwenda na kurudi
skuli. Imeeleza kuwa maeneo hatarishi kama vichaka vilivyo karibu na makazi ya
watu na njia zinazotumiwa na watoto yanapaswa kupunguzwa au kuondolewa ili
kupunguza hatari zinazoweza kuwakabili watoto, hususan wasichana.
Kuhusu uwajibikaji wa taasisi za
haki, TAMWA-ZNZ imesema imekuwa ikishauri Jeshi la Polisi na taasisi nyingine
zinazohusika na haki kutoa taarifa kuhusu hatua zinazofikiwa katika kushughulikia
kesi za ukatili, huku ikizingatiwa sheria na taratibu zinazolinda taarifa nyeti
za waathirika na watoto.
Kwa mujibu wa TAMWA-ZNZ, tangu
mwishoni mwa mwaka 2016 imeshuhudia jumla ya matukio 34 ya mauaji
yaliyowahusisha wanawake 27 na watoto saba, huku jamii ikiwa haijajulishwa
ipasavyo kuhusu mwenendo wa baadhi ya kesi hizo na hukumu zake.
TAMWA-ZNZ pia imeihusisha hali hiyo
na utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs), hususan Lengo la Tano
linalolenga usawa wa kijinsia na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na
wasichana, pamoja na Lengo la 16 linalohimiza jamii zenye amani, upatikanaji wa
haki kwa wote na taasisi zinazowajibika na kufanya kazi kwa ufanisi.
Sambamba na hilo, chama hicho
kimeiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kushirikiana na Wizara ya
Afya kutoa huduma na msaada wa kisaikolojia kwa watoto wanaoishi Kijiji cha
Kwale na maeneo yanayozunguka tukio hilo.
TAMWA-ZNZ imesema msaada huo ni
muhimu kwa watoto ambao wanaweza kuwa wameathirika kwa hofu, msongo wa mawazo
au mshtuko kutokana na tukio hilo, ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila
siku bila kubeba madhara ya muda mrefu ya kisaikolojia.
TAMWA-ZNZ imetoa pole kwa familia,
ndugu, jamaa, walimu na wanafunzi wenzake Raiyan Hemed Amour kufuatia msiba
huo, huku ikiomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi na
kuwapa wafiwa subira na nguvu katika kipindi hiki kigumu.
No comments