Namna Shughuli za Uanikaji Dagaa Mangapwani na Fungurefu Zinavyowadhalilisha Wanawake na Wasichana
NA ABDUL SAKAZA
Ni
saa tisa za usiku katika eneo la Fungurefu, lililopo Shehia ya Mtowapwani,
Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja lenye Wakaazi 3,503, Wanaume
2,041 Nawanawake 1462 kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022. Giza
nene limetanda huku upepo mkali wa bahari ukivuma kwa kasi na kuongeza ukali wa
baridi katika eneo hilo la pwani. Pembeni mwa ufukwe, kundi la wanawake na wasichana
limekusanyika wakinong’ona maneno ya hapa na pale huku wakisubiri kwa hamu boti
za wavuvi zirejee kutoka baharini zikiwa na mzigo wa dagaa.
Baadhi
yao wamejifunika vitenge kujikinga na baridi kali ya usiku, huku wengine
wakitumia mwanga hafifu wa tochi za simu zao kuangaza njia na kuendelea na
shughuli zao katika mazingira yenye changamoto nyingi.
Kila
mmoja anaonekana kuwa na haraka ya kuwahi mzigo wa dagaa kabla haujaisha.
Katika mazingira hayo ya usiku, wanawake hao hulazimika kuvumilia uchovu, hofu
na wakati mwingine vitendo vya udhalilishaji ili tu wapate kipato cha kuendesha
maisha yao.
“Mtu
usipowahi mapema hupati kazi. Tukichelewa tunarudi mikono mitupu,” anasema
mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 19 aliyekubali kuzungumza na mwandishi kwa
sharti la kutotajwa jina lake kwa kuhofia usalama wake.
Katika
ukanda wa pwani wa Kaskazini Unguja, harufu ya dagaa waliokaushwa juani imekuwa
sehemu ya maisha ya kila siku kwa wakazi wa Mangapwani na Fungurefu. Kila
alfajiri wanawake na wasichana huonekana wakikimbilia madikoni wakiwa na ndoo,
mabeseni na vifaa vya kuanikia dagaa kwa matumaini ya kupata kipato kidogo cha
kusaidia familia zao.
Kwa
nje shughuli hizi huonekana kuwa sehemu ya kawaida ya uchumi wa pwani, lakini
nyuma ya pazia kuna simulizi nzito za unyonyaji wa kijinsia, matusi, mazingira
magumu ya kazi na ukosefu wa ulinzi kwa wanawake na wasichana wanaojihusisha na
biashara hiyo.
WAHANGA
WAANIKA MASAIBU YAO
Baadhi
ya wanawake na wasichana wanaofanya kazi ya kuanika na kubeba dagaa katika
maeneo ya Mangapwani na Fungurefu wanasema matukio ya matusi na unyanyasaji wa
kingono yamekuwa yakivunja utu wao na kuwafanya wajisikie kutokuwa salama
katika mazingira yao ya kazi.
Halima
Iddi Juma (si jina lake halisi), anasema Aprili 17, 2025 alifanyiwa udhalilishaji
wa kimwili na mmoja wa wavuvi wakati akisubiri kupokea ndoo ya dagaa karibu na
boti aina ya Ngwanda.
"Aliniingizia
mkono sehemu za siri mbele ya watu. Nilihisi fedheha kubwa sana lakini sikuweza
kuripoti kwa sababu ya aibu na hofu ya namna jamii ingenichukulia,"
anasimulia kwa huzuni.
Mwanamke
mwingine mwenye umri wa miaka 27 kutoka Mangapwani alisema baadhi ya mabaharia
hutumia lugha za matusi na vitisho dhidi ya wanawake wanaokataa mahusiano ya
kingono.
"Ukikataa
wanakwambia hutapata dagaa wa kununua au watakufukuza katika eneo la kazi.
Wengine hutumia nafasi zao kututisha kwa sababu wanajua tunategemea kazi hii
kwa maisha yetu," alisema.
Katika
maeneo hayo pia wapo wasichana walio chini ya umri wa miaka 18 wanaoshiriki
shughuli ndogo ndogo za kuanika na kuchambua dagaa. Baadhi yao wanasema
hukumbana na vitendo vya kushikwa isivyofaa na kutukanwa mara kwa mara, lakini
huendelea kuvumilia kutokana na hali ngumu za kiuchumi na ukosefu wa ajira
mbadala.
Nachia
(si jina lake halisi), mwenye umri wa miaka 16, anasema baada ya kuanza kazi
alipokelewa vizuri, lakini hali ilibadilika baada ya mwajiri wake kuanza
kumtaka kufanya naye ngono.
"Nilifanya
kazi kwa wiki tatu tu. Baadaye mwajiri wangu alianza kunitaka kufanya ngono.
Nilipomkatalia aliniambia niondoke au hatanilipa mshahara wangu. Nililia na
kuwapigia simu watu wa nyumbani. Mwishowe alinilipa na nikatafuta kazi kwa
mwajiri mwingine," alisema.
Uchunguzi
wa mwandishi umebaini kuwa wanawake wengi wanaofanya kazi katika madiko ya
Mangapwani na Fungurefu hawana mikataba rasmi ya ajira wala mifumo madhubuti ya
ulinzi wa haki zao, jambo linalowafanya kuwa katika mazingira yanayoweza
kuchochea unyanyasaji na ukosefu wa haki.
"Tunafanya
kazi kwa hofu kila siku lakini hatuna njia nyingine ya kujipatia kipato. Hii
ndiyo kazi inayotusaidia kuhudumia familia zetu,"
alisema mmoja wa wanawake aliyekutwa akianika dagaa katika eneo la Fungurefu.
Kwa
upande wao, baadhi ya mabaharia, wanunuzi wa dagaa na viongozi wa madiko
waliokubali kuzungumza na mwandishi walikiri kuwepo kwa vitendo vya
udhalilishaji vinavyofanywa na baadhi ya watu katika maeneo hayo, huku
wakisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wahusika na kuimarishwa
kwa mifumo ya kuripoti matukio hayo.
Nahodha
wa boti, Ibrahim Haji, alisema kuwa wanawake wanaofanya kazi za kuanika na
kusindika dagaa wanapaswa kuheshimiwa na kulindwa dhidi ya aina yoyote ya
unyanyasaji.
"Sisi
tunafanya kazi pamoja kila siku na wanawake hawa. Ni wajibu wa kila mmoja
kuhakikisha wanapata mazingira salama ya kufanya kazi. Wale wanaowadhalilisha
wanapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria,"
alisema Ibrahim Haji.
Naye
baharia wa boti, Juma Haji Jecha, alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia
vibaya nafasi zao kwa kuwafanyia wanawake vitendo vya matusi na unyanyasaji
jambo ambalo linapaswa kukemewa na jamii nzima.
"Wanawake
ni sehemu muhimu ya shughuli za dagaa. Hatupaswi kuwanyanyasa wala kuwavunjia
heshima. Tunahitaji kushirikiana kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa
kabisa," alisema Juma Haji Jecha.
Kwa
upande wake, mfanyabiashara wa dagaa Ibrahim Sheha, maarufu kama Kima, alisema
kuwa usalama wa wanawake katika maeneo ya kazi ni muhimu kwa maendeleo ya
biashara na ustawi wa jamii.
"Wanawake
wana mchango mkubwa katika biashara ya dagaa. Wanahitaji kufanya kazi katika
mazingira yenye heshima, usalama na haki bila kuogopa matusi, vitisho au
unyanyasaji wa aina yoyote," alisema Kima.
VIONGOZI
WA MADIKO WAANIKA UKWELI WA MATUKIO
Wasimamizi
wa madiko ya Mangapwani na Fungurefu wanasema matukio ya udhalilishaji dhidi ya
wanawake na wasichana yamekuwa yakiongezeka katika maeneo hayo, hasa wakati wa
usiku ambapo shughuli za upakuaji wa dagaa na uchukuaji hufanyika kwa wingi.
Kwa
mujibu wa viongozi hao, katika mwaka 2025 madiko ya mangapwani na fungurefu
yamenakili kesi 827 sawa na aslilimia
100% ambapo kwa Mangapwani yamenakili jumla ya kesi 240 zinazohusisha wanawake
na wasichana sawa na asilimia 29.0 % ambapo kesi 80 ni za shambulio la matusi sawa
sawa na asilimia 33.3 %. huku kesi 160 zikihusiana na unyanyasaji wa
kingono sawa na asilimia 66.7.
Katika
eneo la Fungurefu, jumla ya kesi 587 sawa na asilimia 71.0 % zimeripotiwa, ambapo kesi 230 ni za
shambulio la matusi , sawa na asilimia
39.2 % na kesi 357 ni za unyanyasaji wa kingono sawa na asilimia 60.8. %
Aliy
Abrahmani Khamisi, ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa diko la Fungurefu, amesema
baadhi ya mabaharia, mapapasi na wafanyabiashara wenye uwezo wa kununua dagaa
wanatajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa katika vitendo vya udhalilishaji dhidi ya
wanawake na watoto wanaojishughulisha na shughuli za uanikaji na biashara ya
dagaa.
"Matukio
mengi hufanywa na baadhi ya mabaharia, mapapasi pamoja na watu wenye uwezo wa
kununua dagaa. Wanawake wengi wanategemea kazi hii kwa ajili ya kujipatia
kipato na kuendesha maisha yao, hivyo mara nyingi hushindwa kujitetea
wanapokumbana na vitendo hivyo," alisema Khamisi.
Kwa
upande wake, Nahodha Haji Meja, kiongozi wa diko la Mangapwani, amesema licha
ya kuwepo kwa idadi kubwa ya matukio ya udhalilishaji, bado kesi nyingi
hazifiki katika vyombo vya sheria kutokana na waathirika kuogopa aibu, vitisho
au kupoteza fursa za kujipatia kipato.
"Wapo
wanawake wanaonyamaza kwa sababu wanaamini wakiripoti wataonekana wasumbufu na
hatimaye kunyimwa nafasi za kufanya kazi katika eneo hili," alisema
Meja.
Kwa
pamoja, viongozi hao wamezitaka mamlaka husika, wadau wa haki za wanawake na
jamii kwa ujumla kuongeza juhudi za kutoa elimu kuhusu haki za binadamu,
kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa za matukio ya ukatili na kuhakikisha
wahusika wa vitendo vya udhalilishaji wanachukuliwa hatua za kisheria ili
kulinda usalama na ustawi wa wanawake na watoto wanaofanya kazi katika sekta ya
dagaa.
|
Jumla ya Kesi |
% ya Kesi Zote |
|
|
Mangapwani |
240 |
29.0% |
|
Fungurefu |
587 |
71.0% |
|
Jumla |
827 |
100% |
RIPOTI
ZA OCGS ZINASEMAJE?
Kwa mujibu wa takuwimu za Ukatili na
Udhalilishaji wa Kijinsia kutoka Ofisi
ya Mkurugenzi Mkuu wa Takwimu Zanzibar (OCGS ya mwaka 2025, jumla ya matukio
1,228 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa Zanzibar, huku
waathirika wakifikia 1,230. Kati ya waathirika hao, watoto walikuwa 1,050 sawa
na asilimia 85.4, wanawake 162 sawa na asilimia 13.2 na wanaume 18 sawa na
asilimia 1.5. Hali hii inaonesha kuwa wanawake na watoto wa kike wanaendelea
kuwa miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi na vitendo vya ukatili wa
kijinsia.
Ripoti
hiyo inaonesha kuwa makosa ya kubaka yaliongoza kwa kuripotiwa mara 660,
yakifuatiwa na matukio ya shambulio la aibu na kukashifu 166, kutorosha 146
pamoja na kulawiti au kunajisi 95. Takwimu hizi zinaashiria kuendelea kuwepo
kwa changamoto kubwa za usalama wa wanawake na watoto katika jamii pamoja na
mazingira mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Aidha,
matukio mengi ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yalitokea nyumbani kwa
mtuhumiwa ambapo yalifikia matukio 574 sawa na asilimia 46.7 ya matukio yote
yaliyoripotiwa. Majumba mabovu yalifuatia kwa matukio 164 sawa na asilimia
13.4. Hali hii inaonesha kuwa maeneo yenye uangalizi mdogo yanaendelea kuwa
sehemu hatarishi kwa wanawake na watoto.
Kwa
upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, ripoti imeonesha kuwepo kwa matukio
mbalimbali ya udhalilishaji wa kijinsia katika wilaya za Kaskazini A na
Kaskazini B, jambo linalodhihirisha kuwa changamoto hiyo bado ipo katika jamii
za mkoa huo na inahitaji juhudi za pamoja za kuzuia na kukabiliana nayo.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa matukio 540 sawa na asilimia 44.0 bado yalikuwa chini ya upelelezi wa Jeshi la Polisi mwishoni mwa mwaka 2025, huku matukio 396 sawa na asilimia 32.2 yakiwa mahakamani. Hali hii inaashiria umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa, uchunguzi na upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.
Hata
hivyo pia kwa mujibu wa taarifa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa
Kaskazini Unguja lenye makao yake Mahonda, baadhi ya matukio ya udhalilishaji
yanayotokea katika maeneo ya Mangapwani na Fungurefu yamekuwa yakiripotiwa
rasmi, ingawa idadi kubwa ya waathirika bado hawajitokezi kutoa taarifa na
ushahidi kwa vyombo husika.
Kwa
mujibu wa ripoti ya polisi iliyotolewa kwa njia ya maandishi kutoka dawati
hilo, jumla ya matukio 118 yaliripotiwa katika maeneo hayo, ambapo matukio 19
ya kushikwa kimwili bila ridhaa yalirekodiwa, sawa na asilimia 16.1. Aidha,
matukio 52 ya lugha za matusi yaliripotiwa, sawa na asilimia 44.1, huku matukio
47 ya unyanyasaji wa kingono yakirekodiwa, sawa na asilimia 39.8 ya matukio
yote yaliyoripotiwa.
“Wanawake
wengi wanaokuja kutoa taarifa husema wamekuwa wakinyanyaswa kwa muda mrefu
lakini waliogopa kuripoti kutokana na mazingira ya kazi zao,” ilieleza sehemu
ya ripoti ya Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Ripoti
hiyo pia imebainisha kuwa wanawake na watoto wa kike ndio wanaoongoza
kuathirika na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia katika maeneo
hayo, hali inayohitaji hatua za haraka za kinga na ulinzi ili kuhakikisha
usalama wao wanapotekeleza shughuli za kujitafutia kipato.
Aidha,
Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kaskazini Unguja limewataka wananchi wa
Mangapwani na Fungurefu kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa
mapema pindi wanaposhuhudia au kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, ili
kurahisisha uchunguzi na kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
Mashirika na taasisi mbalimbali zinazotetea haki za binadamu pamoja na haki za wanawake na watoto Zanzibar zinasema kuwa mazingira ya kazi katika sekta nyingi zisizo rasmi bado hayazingatii kikamilifu usalama, heshima na utu wa mwanamke.
Afisa
Programu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA Zanzibar),
Asia Hakim, amesema wanawake wanaofanya kazi katika maeneo ya mwambao, ikiwemo
shughuli za uvuvi na uanikaji wa dagaa, wanahitaji ulinzi maalumu kutokana na
mazingira wanayofanyia kazi kuwa na vihatarishi vya ukatili na udhalilishaji wa
kijinsia.
Akizungumza
kupitia Mradi wa “Tunaweza Pamoja”, unaotekelezwa na UN Women kwa kushirikiana
na TAMWA Zanzibar kwa ufadhili wa Serikali ya Norway chini ya Mpango wa Pamoja
wa Umoja wa Mataifa unaolenga kujenga jamii salama, yenye usawa na isiyovumilia
ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, Asia alisema bado kuna changamoto ya
wanawake kukosa mifumo salama ya kuripoti matukio ya ukatili.
"Wanawake
hawa mara nyingi hukosa sehemu salama za kutoa malalamiko na wengi wao hufanya
kazi katika mazingira yenye uangalizi mdogo, jambo linalowaweka katika hatari
ya kukumbana na vitendo vya udhalilishaji,"
alisema Asia.
Aidha,
amezitaka taasisi za serikali, viongozi wa jamii, waajiri pamoja na wadau wa
sekta ya uvuvi kushirikiana kuweka mazingira salama ya kazi kwa wanawake,
kuimarisha utoaji wa elimu kuhusu haki za wanawake na kuhakikisha waathirika wa
ukatili wanapata msaada wa kisheria na kisaikolojia kwa wakati.
Kwa
upande mwingine, baadhi ya taasisi zinazojihusisha na utetezi wa haki za
wanawake na watoto ikiwemo JUVIEKA na ZAFELA, zimependekeza kuwepo kwa mifumo
rasmi ya kupokea na kufuatilia malalamiko ya ukatili wa kijinsia katika maeneo
ya madiko, kuongezwa kwa kampeni za elimu ya haki za wanawake pamoja na
kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo ya kazi hususan nyakati za usiku.
Taasisi
hizo zinasema hatua hizo zinaweza kusaidia kupunguza vitendo vya udhalilishaji
na kuwapa wanawake na wasichana nafasi ya kufanya kazi katika mazingira salama,
yenye heshima na yanayolinda haki zao za msingi.
Mamlaka
za Serikali kuptia Afisa Wa Ustawi Wa Jamii Wilaya Ya Kaskazini ‘a’ Makame Khamis
Ali anakiri kuwepo changamoto hizo za vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa
wanawake nawatoto katika maeneo ya Mangapwani na Fungurefu jambo ambalo
linarejesha nyuma ustawi wao na jamii
kwa ujumla
Afisa
Makame ameweka bayana kua wanawake wengi
wanaofanya kazi za kuanika dagaa hutoka katika familia zenye kipato cha chini,
jambo linalowafanya kushindwa kupinga vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa
kutokana na ugumu wamaisha lakini huchukuajuhudi za makusudi kutoa elimu ya
kujitambua katika maeneo hayo .
“Wanawake
hawa wanahitaji kusaidiwa kiuchumi na kupewa elimu ya namna ya kujilinda pamoja
na kuripoti vitendo vya ukatili,” alisema.
Ameongeza
kua baadhi ya waathirika hupata madhara ya kisaikolojia yanayoathiri afya zao
pamoja na mahusiano yao ya kijamii
“Ukatili
wa kijinsia hauishii kwenye maumivu ya mwili pekee, unaacha athari kubwa za
kiakili na kihisia, naiwaombe wazazi na walezi kutowaruhusu Watoto wao Kwenda
katika maeneo hayo kwani ni wadogo sana” aliongeza.
Hali
hiyo inaashiria kuwa licha ya mchango mkubwa wa wanawake katika kukuza uchumi
wa bahari, bado wanakabiliwa na changamoto za usalama na ulinzi wa haki zao
wakiwa maeneo ya kazi.
Vitendo
vya udhalilishaji wa kijinsia vinavyoripotiwa katika maeneo ya Mangapwani na
Fungurefu vinakinzana na matakwa ya sheria za Zanzibar na Tanzania zinazolinda
haki za wanawake na watoto. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 zinatambua haki ya kila mtu
kuishi kwa heshima, usawa na bila kubaguliwa. Aidha, Sheria ya Adhabu Na. 6 ya
mwaka 2018 imeweka adhabu kali kwa makosa yanayohusiana na ubakaji, kulawiti,
unyanyasaji wa kingono na vitendo vingine vinavyokiuka maadili ya jamii.
Vilevile,
Sheria ya Mtoto Na. 6 ya mwaka 2011 ya Zanzibar inamtaka kila mtu kumlinda
mtoto dhidi ya aina zote za ukatili, unyanyasaji, udhalilishaji na matumizi
mabaya.
Hata hivyo, ushahidi uliokusanywa katika
uchunguzi huu unaonesha kuwa licha ya kuwepo kwa sheria hizo, wanawake na
wasichana wanaofanya kazi katika maeneo ya mwambao bado wanakumbana na vitendo
vya matusi, vitisho na unyanyasaji wa kingono vinavyohatarisha usalama wao na
kuvunja haki zao za msingi
Je,
haya yatadumu mpaka lini? Wakati dagaa linaendelea kuwa chanzo cha kipato kwa
mamia ya familia za pwani, wanawake wengi wanaolinda uchumi huo wanaendelea
kubeba maumivu kimya kimya wakisubiri siku ambayo sauti zao zitasikika na haki
zao kulindwa.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

No comments