Breaking News

Wananchi Watakiwa Kufuata Sheria Ugawaji wa Mirathi Kuzuia Dhulma na Migogoro

NA SAFIA MOHAMED.

WANANCHI wametakiwa kufuata taratibu za kisheria katika ugawaji wa mirathi kwa kufika katika mamlaka husika ili kuhakikisha haki za warithi wote zinalindwa na kuepusha migogoro, ubaguzi na dhulma zinazoweza kujitokeza wakati wa kugawana mali za marehemu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Dk. Sikujua Omar Hamdan, alisema hayo wakati akitoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi wa Uzini, Wilaya ya Kati, Unguja, katika hafla iliyofanyika Skuli ya Uzini.

Dk. Sikujua alisema baadhi ya watu wamekuwa wakigawana mirathi kwa kufuata uelewa wao binafsi au hisia zao bila kuzingatia taratibu zinazotakiwa kisheria, hali inayoweza kusababisha baadhi ya warithi kunyimwa haki zao.

Alisema ni muhimu kwa wananchi kufika katika taasisi na mamlaka zinazohusika na masuala ya mirathi ili kupata mwongozo sahihi wa kisheria kabla ya kufanya ugawaji wa mali za marehemu.

Alifahamisha kuwa kufuata taratibu hizo kutasaidia kuhakikisha kila mrithi anapata haki yake kwa mujibu wa sheria zinazotumika, pamoja na kupunguza uwezekano wa kutokea kwa migogoro ya kifamilia inayoweza kuathiri uhusiano wa ndugu na jamaa.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kujisomea na kutafuta elimu ya sheria ili kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu wao, akieleza kuwa ufahamu wa masuala ya kisheria ni nyenzo muhimu katika kujilinda dhidi ya vitendo vya dhulma.

Kwa upande wake, Ofisa Sheria kutoka Kituo cha Huduma za Kisheria Zanzibar (ZLSC), Siima Nyakaosa Bagoka, alieleza umuhimu wa wananchi kupata elimu ya kisheria ili waweze kutambua haki zao na kujua hatua za kuchukua wanapokabiliwa na changamoto zinazohitaji msaada wa kisheria.

Alisema elimu hiyo ni muhimu katika kuijengea jamii uelewa wa masuala ya sheria na kuwawezesha wananchi kutafuta msaada kutoka katika taasisi zinazohusika badala ya kufanya maamuzi bila mwongozo unaofaa.

Naye Ofisa Ustawi kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Nassor Haji Juma, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na uelewa wa masuala ya kisheria na kijamii, akibainisha kuwa elimu hiyo inaweza kusaidia kuimarisha mahusiano katika familia na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Sheria kutoka Uzini, Mwaka Abdulrahman, alieleza umuhimu wa wananchi kutumia huduma za msaada wa kisheria wanapokabiliwa na changamoto zinazohusu haki zao, ikiwemo masuala ya mirathi, ili kupata ushauri na mwongozo unaofaa.

Naye Sheha wa Uzini, Abubakar Othman Khamis, alieleza umuhimu wa wananchi kushiriki katika shughuli za utoaji wa elimu ya kisheria zinazolenga kuongeza uelewa wao kuhusu sheria na namna zinavyoweza kutumika katika kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walieleza umuhimu wa elimu hiyo katika kuwasaidia kuelewa masuala ya kisheria yanayohusu maisha yao na namna ya kutafuta msaada wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali.

Elimu hiyo imetolewa kupitia Mradi wa Kliniki ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid Clinic), unaoendeshwa na Kituo cha Huduma za Kisheria Zanzibar (ZLSC), kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mradi huo unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sheria na masuala ya kisheria yanayogusa maisha yao ya kila siku, pamoja na kuwasaidia kufahamu haki zao na mahali pa kupata huduma za msaada wa kisheria wanapozihitaji.


No comments