Breaking News

Mh. Khadija Salum Ali, Aipongeza Africa Leaf Kutoa Msaada Vifaa vya Shule.



Na Khadija Ali.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Khadija Salum Ali, amewataka wadau wa maendeleo kuendelea kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwawezesha kupata mahitaji muhimu ya elimu na kuwajengea matumaini ya maisha bora.

Alisema hayo katika hafla ya kugawa mikoba ya skuli na madaftari kwa watoto hao kutoka mikoa yote ya Unguja, msaada uliotolewa na Taasisi ya Africa Leaf and Community Development kupitia programu ya kuwarejesha watoto skuli.
Khadija alisema misaada hiyo inaongeza upendo, mshikamano na faraja kwa watoto, huku ikiwaonesha kuwa wanathaminiwa na jamii na wana haki ya kupata elimu kama watoto wengine.

Alieleza kuwa upatikanaji wa vifaa vya skuli ni hatua muhimu katika kupunguza changamoto zinazoweza kuwazuia watoto wenye uhitaji kuendelea na masomo yao.
Aliwataka wazazi na walezi wa watoto waliopokea msaada huo kuhakikisha wanavitunza na kuvitumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili viwasaidie katika safari yao ya elimu.

Aidha, alisema ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kupunguza mzigo wa mahitaji kwa familia zenye uhitaji na kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa za kujifunza.

Aliiomba Africa Leaf and Community Development kuendelea na juhudi zake za kusaidia jamii, huku akiwahimiza wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo ili kuwafikia watoto wengi zaidi wanaohitaji msaada.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Africa Leaf and Community Development, Muhammad Gewily, alisema taasisi hiyo imefanikiwa kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na kutoa misaada ya kibinadamu nchini Tanzania katika miaka iliyopita.



Alisema taasisi hiyo inaendelea kupanua wigo wa shughuli zake, ikiwemo kusaidia elimu na kujenga vituo vya elimu, kwa lengo la kuwafikia watu wengi zaidi wenye mahitaji.
Gewily alieleza kuwa taasisi hiyo inalenga kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Jamii ili kutekeleza kwa ufanisi shughuli za maendeleo na misaada ya kibinadamu.
Alisema kufanya kazi kwa pamoja na serikali pamoja na wizara husika kutasaidia kuimarisha huduma kwa jamii na kufanikisha malengo ya kuwasaidia watu wenye uhitaji.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Hifadhi ya Mtoto, Mkasi Abdalla Rajab, aliwahimiza wadau wengine kuendelea kutoa misaada kupitia Wizara, ambayo inaratibu masuala ya watoto wenye uhitaji, ili kuhakikisha wanapata ulinzi, msaada na faraja.
Kwa upande wao, wazazi na walezi wa watoto waliopatiwa msaada huo waliwashukuru wafadhili kwa kuwasaidia kupata vifaa vya skuli, wakisema hatua hiyo itapunguza gharama za mahitaji ya watoto wao na kuwawezesha kuendelea na masomo.

Waliomba wadau waendelee kutoa misaada hiyo kwa moyo wa kujitolea, wakieleza kuwa usaidizi wa mahitaji ya msingi ya elimu ni muhimu katika kuwapa watoto wenye mazingira magumu nafasi ya kujenga maisha bora ya baadaye.

2 comments: