Breaking News

Tuungane Kuimarisha Biashara Zanzibar. RC Mo'hd Ali Abdalla.


Na Khadija Ali
.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Moh'd Ali Abdallah, amewataka wadau wa maendeleo ya mji wa Zanzibar kushirikiana katika kuimarisha shughuli za biashara, usafi na utunzaji wa mazingira ili kuufanya mji huo kuwa wa kisasa, wenye kuvutia na kutoa mazingira bora kwa wakazi na wageni.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na wadau hao Ofisini kwake Vuga, Alisema ukuaji wa biashara na maendeleo ya wafanyabiashara ni miongoni mwa nguzo muhimu ya maendeleo ya mji, hivyo ni lazima kuweka mazingira yanayowawezesha kufanya shughuli zao kwa utaratibu na kuzingatia  usafi, mpangilio na mwonekano mzuri wa maeneo ya biashara.

Aidha alisema ni muhimu wa kushirikiana kuboresha mandhari ya Zanzibar na kuimarisha usafi wa maeneo ya umma, kutunza mazingira na kupendezesha maeneo mbalimbali ya mji ili yaendane na mahitaji ya maendeleo ya kisasa.

Alisema uboreshaji wa miundombinu ya barabara na maeneo ya biashara unaweza kuongeza mvuto wa mji na kuuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa miji inayotambulika kwa upekee wake katika Afrika Mashariki.

Mkuu Moh'd alisema Aidha, juhudi za kuendeleza mji haziwezi kufanikiwa bila kuwepo kwa amani, utulivu na usalama hivyo  aliwataka wadau wote kutekeleza wajibu wao katika kulinda hali hiyo na kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi zinaendelea katika mazingira salama.

Hata hivyo alisema ni vyema  wafanyabiashara, taasisi za serikali na wadau wengine kuunganisha nguvu katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya mji, badala ya kuiachia serikali pekee jukumu la kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na yenye kuvutia.

Hivyo alihimiza kila mdau kuwajibika katika eneo lake kwani aushirikiano wa pamoja ndio msingi wa kufanikisha azma ya kuifanya Zanzibar kuwa mji wenye maendeleo, biashara imara, mazingira bora na mwonekano unaovutia wakazi na wageni.

Nao wadau hao waliahidi kushirikiana na serikali ili kuhakikisha kila mwananchi anatekeleza wajibu wake wa kusafisha mazingira ili Zanzibar iendelee kuwa safi, salama na kupendeza.

1 comment: