ZDCEA, Posta Tanzania kushirikiana Kudhibiti Usafirishaji Dawa za kulevya Zanzibar.
Na Siti Ali.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) imesaini Hati ya Makubaliano na Shirika la Posta Tanzania kwa lengo la kuimarisha udhibiti na ukaguzi wa nyaraka, vipeto, vifurushi na mizigo inayosafirishwa kupitia mtandao wa posta, ambao umebainika kutumiwa na baadhi ya wahalifu kama njia ya kusafirisha dawa za kulevya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Anna Athanass Paul amezitaka taasisi hizo kutekeleza makubaliano hayo kikamilifu na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kupima utekelezaji na mafanikio yake.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imejizatiti kupambana na janga la dawa za kulevya kwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zinazohusika katika kudhibiti na kuzuia usafirishaji wa dawa hizo.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa ZDCEA, Kanali Burhan Zuberi Nassoro, amesema mbinu zinazotumiwa na wahalifu katika kusafirisha dawa za kulevya zimeendelea kubadilika, kutoka njia za kawaida hadi kutumia mifumo ya posta na biashara ya kidijitali.
Amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa vifurushi na mizigo, kulinda maisha ya wananchi pamoja na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa Shirika la Posta ambao wako mstari wa mbele katika kutoa huduma hizo.
Naye Postamasta Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Daniel Mbodo, amesema makubaliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Posta Duniani unaohimiza usalama na ushirikiano katika utoaji wa huduma za posta.
Amesisitiza kuwa mtandao wa posta unapaswa kuwa salama kwa watumiaji wote, huku akionya watu wanaojaribu kuutumia kusafirisha dawa za kulevya kuwa watabainika na kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Aidha, viongozi hao wamekubaliana kuimarisha utoaji wa elimu kwa wadau na wananchi, kubadilishana taarifa kwa utaratibu maalumu na kuongeza ushirikiano katika ukaguzi wa nyaraka, vipeto, vifurushi na mizigo inayopitia mtandao wa posta.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa ufanisi na kuchangia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuifanya Zanzibar kuwa salama dhidi ya biashara na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya
Hati hiyo ya makubaliano imesainiwa leo Oktoba 29,2026 katika ofisi za ZDCEA, Migombani, Zanzibar, katika hafla iliyoshuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Anna Athanass Paul, Kamishna Mkuu wa ZDCEA, Kanali Burhan Zuberi Nassoro, pamoja na Postamasta Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Daniel Mbodo, na watendaji wa taasisi hizo mbili.

.jpeg)
.jpeg)
muhimu sana
ReplyDelete