Breaking News

SERIKALI KUIMARISHA SEKTA YA SHERIA NA HAKI ZANZIBAR


NA SITI ALI.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha sekta ya sheria na haki ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, huku ikitambua mchango mkubwa wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika kusimamia haki jinai, kulinda maslahi ya umma na kuimarisha utawala wa sheria nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakati wa maadhimisho ya miaka 24 tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Madinat Al Bahr, Mbweni.

Mhe. Hemed amesema uwepo wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka umeimarisha mfumo wa haki jinai kwa kuweka mgawanyo sahihi wa madaraka kati ya taasisi za sheria na kuongeza imani ya wananchi kwa vyombo vya dola. Amesema mfumo huo pia umechangia kujenga mazingira salama yanayowezesha uwekezaji na maendeleo ya uchumi.

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuziimarisha taasisi za haki ili ziweze kukabiliana na ongezeko la uhalifu wa kisasa, ikiwemo rushwa, dawa za kulevya, uhalifu wa kimtandao, utakatishaji wa fedha haramu pamoja na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali imeweka zaidi ya shilingi bilioni 13.6 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mahakama, kuimarisha mifumo ya TEHAMA na vitendea kazi, sambamba na kuboresha maslahi ya watumishi wa sekta ya sheria na kuwajengea uwezo waendesha mashtaka na wapelelezi ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa haki.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman, amesema Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka na kuwataka waendesha mashtaka kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazopambana na rushwa, uhujumu uchumi na dawa za kulevya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Mhe. Mgeni Jecha Jailani, amesema katika kipindi cha Awamu ya Nane ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa ikiwemo kufanyiwa marekebisho kwa sheria za haki jinai, kuimarika kwa ushirikiano kati ya taasisi za haki jinai na kuanzishwa kwa mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za mashtaka.

Hata hivyo, Mhe. Jailani amesema ofisi hiyo bado inakabiliwa na changamoto za uhaba wa majengo, vitendea kazi na uboreshaji wa maslahi ya waendesha mashtaka. Ameeleza kuwa kushughulikia changamoto hizo kutaiwezesha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuendelea kutoa huduma bora zaidi na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.


1 comment: