Breaking News

MARIDHIANO YA CCM NA ACT WAZALENDO YAFUNGUA NJIA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFAMZANZIBAR.

 


NA SITI ALI.

Zanzibar imeandika ukurasa mpya katika historia yake ya kisiasa baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo kuwasilisha Tamko la Pamoja na kusaini Ajenda za Kuchukuliwa Hatua, hatua inayolenga kuimarisha maridhiano na kufungua njia ya utekelezaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hafla hiyo ilifanyika katika Viwanja vya Ikulu Zanzibar, tarehe 9 Julai 2026, ikihudhuriwa na viongozi wakuu wa kitaifa, wadau wa maendeleo na wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alisema kuwa tamko hilo ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya viongozi wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar badala ya tofauti za kisiasa. Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha amani, umoja, mshikamano na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu.

Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza kuwa maridhiano hayo si suala la kisiasa pekee bali ni fursa ya kujenga utawala bora, kuongeza uwajibikaji, kuimarisha utoaji wa haki na kuendeleza utengamano wa kijamii. Alibainisha kuwa mafanikio ya mchakato huo yataongeza imani ya wananchi, wawekezaji na washirika wa maendeleo katika mustakabali wa Zanzibar.

Aidha, aliwahakikishia viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kuwa ataendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatekelezwa kwa ufanisi. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo, kujenga kuaminiana, kuheshimiana na kuvumiliana ili kulinda amani na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliipongeza Zanzibar kwa kufikia hatua hiyo ya kihistoria, akieleza kuwa maridhiano hayo yanafungua ukurasa mpya wa kuimarisha umoja, utulivu na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari. Alisema hatua hiyo inaonyesha ukomavu wa kisiasa na dhamira ya viongozi kujenga mazingira bora ya amani na maendeleo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi wake katika kuendeleza mazungumzo hayo. Alisema makubaliano yaliyofikiwa yanaweka msingi wa kupata suluhisho la kudumu kwa changamoto za kisiasa ambazo zimekuwa zikiikabili Zanzibar kwa muda mrefu.



Katika hafla hiyo, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Maridhiano, aliwasilisha Tamko la Pamoja kabla ya kufanyika kwa utiaji saini wa Ajenda za Kuchukuliwa Hatua. Chama Cha Mapinduzi kiliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, huku ACT Wazalendo ikiwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wake, Omar Ali Shehe.

Tukio hilo lilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Marais Wastaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, mabalozi, taasisi za kimataifa pamoja na wananchi. Wito ulitolewa kwa Watanzania wote kuunga mkono maridhiano hayo ili yawe msingi wa kudumisha amani, demokrasia na maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.


No comments