USHIRIKISHWAJI WA WATU WENYE ULEMAVU NI CHACHU YA UTAWALA BORA
Na Siti Ali
Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Awamu ya Tano (CEJG Phase V), unaotekelezwa na Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Kanda ya Zanzibar, umeendelea kuhamasisha ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika ngazi mbalimbali za maamuzi kama sehemu ya kuimarisha utawala bora na maendeleo jumuishi katika jamii.
Kupitia mafunzo, mikutano ya jamii na shughuli za uhamasishaji zinazotekelezwa katika Wilaya ya Kaskazini 'B', mradi huo unalenga kuongeza uelewa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, kuwajengea uwezo viongozi wa shehia pamoja na wananchi, na kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo na maamuzi yanayowahusu.
Wilaya ya Kaskazini 'B' ni miongoni mwa wilaya zinazokuwa kwa kasi kupitia shughuli za kilimo, uvuvi na utalii. Hata hivyo, mafanikio ya maendeleo hayawezi kuwa endelevu bila kuhakikisha makundi yote ya jamii, hususan watu wenye ulemavu, yanashiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo.
Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Awamu ya Tano kutoka Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Kanda ya Zanzibar, Msafiri Thomas Mombo, amesema kuwa mradi unaweka mkazo katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika masuala ya haki na utawala bora.
"Utawala bora unahitaji ushiriki wa kila mwananchi. Kupitia mradi huu tunaendelea kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapatiwa nafasi sawa katika kamati za uongozi wa shehia, wanashiriki katika mijadala ya maendeleo na wanapata fursa ya kutoa maoni yao. Hii ndiyo njia sahihi ya kujenga jamii yenye uwajibikaji, uwazi na usawa," amesema Mombo.
Sheha wa Shehia ya Mahonda Mkataleni, Mohammed Suleiman Mohammed, amesema mafunzo yaliyotolewa kupitia mradi huo yameongeza uelewa wa viongozi kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli zote za maendeleo.
"Utawala bora unajidhihirisha pale ambapo rasilimali za umma, mipango ya maendeleo na fursa za kiuchumi zinagawiwa kwa usawa bila ubaguzi. Kupitia elimu hii tunaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wote, wakiwemo watu wenye ulemavu, wanashiriki katika maamuzi ya maendeleo ya shehia," amesema.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini 'B', Shaaban Sariboko Makarani, amesema ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu husaidia kupanga maendeleo yanayozingatia mahitaji halisi ya wananchi.
Ameeleza kuwa ushiriki wao katika Kamati za Maendeleo za Shehia na vyombo vingine vya maamuzi huwezesha serikali kupanga miundombinu rafiki kama njia maalumu za kupita, vyoo vinavyofikika kwa urahisi na huduma nyingine muhimu tangu hatua za awali za utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake, Mchungaji Emmanuel Malingila wa Shehia ya Kitope amesema elimu inayotolewa kupitia mradi huo imechangia kupunguza unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu na kuongeza ushirikiano katika jamii.
"Kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika ajira, mafunzo ya amali na shughuli nyingine za maendeleo kunajenga jamii inayoheshimu utu wa kila mtu. Huo ndio msingi wa haki za binadamu na utawala bora," amesema.
Sheikh na Imamu wa Shehia ya Mahonda, Salum Gharib Salum, amesema viongozi wa dini wana wajibu wa kuendelea kuielimisha jamii kuhusu usawa na haki za watu wenye ulemavu.
"Hakuna maendeleo ya kweli kama watu wenye ulemavu wataendelea kutengwa. Lazima washiriki katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla," amesema.
Wanufaika wa mradi huo pia wameeleza mafanikio na changamoto wanazokutana nazo.
Abdallah Saleh Salum, ambaye ni mtu mwenye ulemavu wa kusikia kutoka Shehia ya Donge Majenzi, amesema mafunzo aliyoyapata kupitia mradi yamemjengea uwezo wa kutambua haki zake na kushiriki katika shughuli za kijamii.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto za ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama katika mikutano ya umma, pamoja na kukosekana kwa takwimu sahihi za watu wenye ulemavu katika baadhi ya shehia.
"Tunahitaji kuona wakalimani wa lugha ya alama katika mikutano ya serikali na kuwepo kwa kanzidata sahihi ya watu wenye ulemavu ili mipango ya maendeleo izingatie mahitaji yetu," amesema.
Naye Rehema Haji Seif, ambaye pia ni mnufaika wa mafunzo ya mradi huo, amesema elimu aliyoipata imemwezesha kuwa mtetezi wa haki za watu wenye ulemavu katika jamii yake.
Amesema kuna umuhimu wa kufanya utambuzi wa watu wenye ulemavu katika kila shehia, kuboresha huduma za usafiri na kusogeza mikutano ya maendeleo karibu na wananchi ili kuongeza ushiriki wao.
Sheha wa Shehia ya Mahonda, Ali Issa Kinole, amesema mafunzo yaliyotolewa kupitia Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Awamu ya Tano yameongeza uelewa wa viongozi kuhusu wajibu wao wa kusimamia utekelezaji wa sera na sheria zinazolinda haki za watu wenye ulemavu.
"Ni wajibu wa taasisi zote kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki sawa katika huduma za umma na binafsi. Ushirikishwaji wao ni sehemu muhimu ya maendeleo endelevu," amesema.
Mradi huo pia unaendelea kuhamasisha uwezeshaji wa kiuchumi kwa watu wenye ulemavu kupitia vikundi vya uzalishaji, mafunzo ya biashara na uhusiano na taasisi za kifedha ili kuongeza uwezo wao wa kujitegemea kiuchumi.
Aidha, mradi unasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwakilishi wa watu wenye ulemavu katika kamati mbalimbali za maendeleo za shehia na wilaya ili kuhakikisha sauti zao zinazingatiwa katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kupitia utekelezaji wa Mradi wa Uwezeshaji wa Jamii kwa Ajili ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Awamu ya Tano, Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Kanda ya Zanzibar inaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali, viongozi wa dini, mashirika ya kiraia na wananchi katika kujenga jamii inayozingatia haki za binadamu, usawa na utawala bora.
Ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu si suala la hiari bali ni msingi wa maendeleo jumuishi. Kuimarisha ushiriki wao katika maamuzi, utekelezaji wa miradi na uongozi kutaiwezesha Wilaya ya Kaskazini 'B' kuwa mfano wa kuigwa katika kujenga jamii yenye haki, usawa na ustawi kwa wananchi wote.

No comments