Breaking News

JUKUMU LA KUPAMBANA NA RUSHWA SIO LA ZAECA NA TAKUKURU PEKEE TUWAJIBIKE KILA MMOJA KWA NAFASI YAKE. MAKAMU WA PILI WA RAIS.



Na SITI ALI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi kwa lengo la kukuza uadilifu na kupambana na Rushwa nchini.

Hayo yameelezwa  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla  kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi  katika hafla ya maadhimisho ya siku ya mapambano dhidi ya Rushwa Barani Afrika yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

Amesema katika mapambano dhidi ya Rushwa na uhujumu uchumi nchini hatua mbalimbali zimechukuliwa kama vile kuanzishwa kwa Tume za Maadili ya Viongozi wa Umma, kuanzishwa kwa Taasisi maalum za kupambana na rushwa pamoja na kuimarisha sheria mbali mbali zikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Sura 338 ya Tanzania Bara na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma nambari 4 ya mwaka 2015, Zanzibar. 

Mhe. Hemed amesema  sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa nambari 11 ya mwaka 2007 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar nambari 5 ya mwaka 2025 zimeimarishwa  sambamba na Sheria ya ununuzi wa Umma nambari 2 ya mwaka 2025 na Sheria ya ukaguzi wa Umma nambari 7 ya mwaka 2025.



Aidha, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amesema Tanzania inaendelea kuhakikisha kuwa Mikataba yote ya Kikanda na Kimataifa inayohusu mapambano dhidi ya rushwa unatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Taifa jambo lililosaidia ZAECA kuokoa na kurejezha hazina zaidi ya Bilioni 5 pamoha na Dola za Kimarekani 398 kwa kipindi cha mwezi Julai 2025 hadi Mei 2026 zilizopatikana kutokana na kudhibiti ubadhilifu, ukwepaji wa kodi na matumizi mabaya ya madaraka.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa si jukumu la ZAECA na TAKUKURU pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja kusimamia uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake kwa nafasi aliyonayo na kusema kuwa ushirikiano wa pamoja kati ya wanachama, wananchi, viongozi, sekta binafsi na taasisi za kiraia utawezesha kushinda vita dhidi ya rushwa.



Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu Uchumi Zanzibar ( ZAECA ) ndugu ALI ABDALLA ALI amesema katika kufikia adhma ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar katika kudhibiti rushwa na uhujumu uchumi nguvu za pamoja zinahitajika ili kuwa na Taifa salama lisilo na mianya ya rushwa na uhujumu uchumi.

Ndug ALI  amesema ZAECA kwa kushirikiana na TAKUKURU  wanafanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kutoa huduma bora zisizo na malalamiko ya uwepo wa rushwa na uhujumu uchumi nchini.

Akitoa Salamu za Taasisi ya kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bwana CRISPIAN F. CHALAMILA amesema rushwa dhidi ya uhujumu uchumi imekuwa ni kikwazo kikubwa katika jamii na kuleta athari mbalimbali za kiuchumi na kijamii, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika katika mapambano dhidi ya rushwa.



Mapema Makamu Mwenyeki wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Afrika ya kupinga Rushwa Bibi IVONA MUTEPUKI  ACHIBIA amesema wakati umefika kwa Taasisi za Kupambana na rushwa kutoa elimu zaidi ya mapambano dhidi ya rushwa kuanzia ngazi za chini na kuifikia jamii moja kwa moja ili iwe na uwelewa moana juu ya athari za kutoa na kupokea rushwa.

Bibi IVONA amesema kuadhimisha siku ya mapambano dhidi ya rushwa iwe ni meanzo mzuri wa viongozi kuweka mikakati, kujitoa na kuwa na utayari thabiti wa kupambana na  kuitokomeza rushwa Zanzibar, Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla.


No comments