NAIBU KATIBU MKUU ELIMU AAGIZA BODI ZA ELIMU KUIMARISHA UFUATILIAJI MAENDELEO YA SKULI.
NA SAID KHAMIS
Naibu Katibu Mkuu (Utawala) wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Amos John Hwnock, amewataka wajumbe wa Bodi za Elimu za Mikoa na Wilaya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ufuatiliaji wa karibu ili kuinua kiwango cha elimu nchini.
Ndg. Hwnock ametoa agizo hilo wakati akifungua kikao maalumu cha kutathmini utendaji wa kazi kwa muhula wa kwanza wa masomo kilichowashirikisha wajumbe wa bodi hizo huko katika ukumbi wa Skuli ya Maandalizi Madungu, Chake Chake Pemba.
Katika hotuba yake, Naibu Katibu Mkuu amebainisha kuwa ili kurahisisha utendaji kazi wa bodi hizo, wajumbe watatengewa bajeti maalumu itakayosaidia kufanikisha ufuatiliaji na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi zaidi.
Akigusia masuala ya kitaaluma Maskulini, Hwnock amepiga marufuku tabia ya baadhi ya walimu kuwalazimisha wanafunzi kusoma masomo ambayo si chaguo lao, akisisitiza kuwa hatua hiyo inafifisha vipaji na ari ya Wanafunzi kufanya vizuri.
Aidha, amewasihi wazazi na walezi nchini kuwa karibu na watoto wao kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo yao ya kitaaluma na nidhamu wanapokuwa nje ya Skuli.
Kwa upande wake, Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwalimu Mohamed Nassor Salim, amewashauri wajumbe hao kutoficha changamoto zinazowakabili, bali waziwasilishe kwa uwazi ili kupata suluhu ya pamoja inayokwamisha harakati za maendeleo ya Elimu katika maeneo yao.
Katika kikao hicho, Mratibu Idara ya Elimu Sekondari, Bi. Tarehe Khamis Hamad, amewasilisha ripoti ya ufuatiliaji wa utendaji kazi na kuzitaja changamoto kuu nne zinazochangia kuathiri vibaya matokeo ya mitihani ya wanafunzi.
Changamoto hizo ni pamoja na Ukosefu wa utayari miongoni mwa wanafunzi wenyewe katika kujisomea, Ufuatiliaji duni wa maendeleo ya wanafunzi kutoka kwa wadau wa elimu na wazazi, Kushuka kwa motisha kwa walimu na wanafunzi katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji na Uhaba wa walimu unaokabili baadhi ya skuli.
Kikao hicho cha tathmini kimeleta pamoja wadau mbalimbali wa elimu Kisiwani Pemba kwa lengo la kuweka mikakati thabiti itakayosaidia kutatua changamoto hizo na kuongeza ufaulu katika mitihani ya kitaifa.






No comments