NA SITI ALI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameikaribisha Sweden kuongeza uwekezaji Zanzibar, akisema Serikali imeweka mazingira rafiki yanayowezesha wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo nishati, kilimo cha mwani na uchumi wa buluu.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Julai 14, 2026, alipokutana na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.
Amesema Zanzibar inaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta ya nishati kwa kuwekeza katika vyanzo mbadala vya umeme, hususan nishati ya upepo na jua, na kuyakaribisha makampuni ya Sweden kushiriki katika juhudi hizo ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa umeme na kuifanya Zanzibar kujitegemea zaidi.
Akizungumzia uchumi wa buluu, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeweka mkazo katika kuendeleza zao la mwani kwa kuliongezea thamani kupitia usindikaji wa bidhaa mbalimbali badala ya kuendelea kulisafirisha kama malighafi, hatua inayolenga kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya zao la mwani na kuvutia uwekezaji utakaowezesha maendeleo ya viwanda vya usindikaji, ili wananchi wanufaike zaidi na rasilimali zilizopo nchini.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameishukuru Serikali ya Sweden kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika kusaidia maendeleo ya Zanzibar, hususan kupitia sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii, na kuiomba kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.
Kwa upande wake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi na wananchi wa Zanzibar kwa hatua ya uwasilishaji wa Tamko la Pamoja pamoja na utiaji saini wa Ajenda za Kuchukuliwa Hatua kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo.
Amesema hatua hiyo ni ishara ya kuimarika kwa maridhiano ya kisiasa na utulivu nchini, jambo ambalo linaendelea kuijengea Zanzibar mazingira mazuri ya maendeleo, ushirikiano wa kimataifa na kuvutia uwekezaji kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Sweden.



No comments