VIJANA WAMETAKIWA KUONGEZA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA ILI UWEZE KUPUNGUA.
NA SITI ALI.
Akizungumza na wandishi wa Habari huko katika tamasha la sauti za busara lililofanyika huko Mpendae Mratibu wa mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na waschana kutoka UN WOMEN kanda ya Zanzibar Lucy Tesha Amesema kuwa, tamasha hilo limewalenga wanafunzi wa vyuo vikuu vya Zanzibar kutoa ujumbe wa ukatili wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kuwa viongozi na kuwa, ushiriki wa vijana katika tamasha hilo ni mkubwa na wao ndiyo wameshiriki pakubwa katika maandalizi ya tukio hilo la kihistoria.“ Lazima tukubali vijana ndiyo wenye nguvu za Mabadiliko katika jamii zetu na taifa kwa ujumla ni vyema kuwashirikisha katika kila sekta ili kuleta maendeleo kwa haraka “ amesema Lucy.
Nae, Zakia Lulu ambae Mratibu wa Tamasha la Sauti za Busara Zanzibar , amesema lengo la Tamasha hilo kuhamasisha wanawake na mtoto wake kuja kuwa viongozi bora na sio lazima wafanye kazi Serikalini bali waazie katika ngazi za chini , mitaani au katika mashule. “ Tunataka Watoto wa kike waanze kuchukuwa nafasi za Uongozi wakiwa nafasi za shule au vyuo vikuu wakiona kuna nafasi ya wao kuongoza basi wafanye hivyo” amesema Zakia.
Aidha Amesema kuwa, Takwimu za ukatili na Udhalilishaji wa kijinsia zinatisha , msichana mmoja kati ya watatu wameolewa kabla ya umri wa miaka 18, asilimia 17 ya wanawake wa Tanzania wanapitia udhalilishaji wa kijinsia bado wadau wanaendelea kuzungumzia unyanyasaji wa kijinsia.“Kwa kweli inaumiza imefika pahali kila mmoja aone ana nafasi ya kufanya kitu ili kutokomeza vitendo hivi, ndiyo maana tumeona tuwaze na wanafunzi wa vyuo kuwashirikisha ipasavyo ili waweze kujitambua na kujikinga” amesema Zakia.
Hata hivyo amesema kuwa, vijana wa Sekondari na Vyuo ndiyo wako katika hatari zaidi a kujiingiza katika vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwani wengi wao wanahisi wamekuwa wanaweza kujiamulia chochote wasipokuwa na tahadhari wanaweza kujiingiza katika vitendo vya udhalilishaji.
Nao wanafunzi wa vyuo walioshiriki katika Tamasha hilo Fatma Kassim na Abubakar Yasin wamesema kuwa, ni vyema matamasha kama hayo kuendelea kuwepo kwa lengo la kutoa elimu mbali mbali na kuwashirikisha vijana kuweza kujitambua.Wamesema kuwa, vijana wa chuo hukumbana na changamoto mbali mbali na muda mwengine huathiri masomo yao na kupelekea kushindwa kutimiza ndoto zao za kielimu, hivyo wamewashukuru waandaaji wa Tamasha hilo kwa kuwapatia elimu za udhalilishaji. Tamasha hilo la Sauti za Busara ni mara ya nne kufanyika , kwa mara hii limefanyika kwa kuwashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu na Sekondari na likiwa na ujumbe wa usemao ‘Mabadiliko yanaanza na mimi ‘


No comments