Breaking News

MASHEHA PEMBA WAJENGEWA UELEWA WA KULINDA BAHARI NA KUKABILIANA NA UVUVI HARAMU.



Na Juma Seif 

 Jamii imetakiwa kushirikiana kikamilifu katika kukabiliana na vitendo vinavyosababisha uharibifu wa mazingira ya bahari ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinaendelea kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Wito huo umetolewa katika mkutano wa kuwajengea uwezo Masheha wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kuhusu uvuvi usiokubalika na mbinu za kulinda mazingira ya bahari.

Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Pemba, Omar Juma Suleiman, amesema kuwa uhifadhi wa mazingira ya bahari ni msingi wa kuendelea kwa maisha ya viumbe wa baharini na ustawi wa sekta ya uvuvi.

Alieleza kuwa mifumo ikolojia ya bahari, ikiwemo mikoko, nyasi bahari na matumbawe, ina mchango mkubwa katika kuzaliana kwa samaki na viumbe wengine wa baharini, hivyo uharibifu wake unatishia usalama wa chakula, kipato cha wavuvi na maendeleo ya uchumi wa buluu.



"Bila ya mikoko, nyasi bahari na matumbawe, hakuna mazingira salama ya viumbe wa baharini kuishi na kuzaliana. Hivyo, sote tuna wajibu wa kulinda rasilimali hizi ili kuhakikisha tunakuwa na bahari endelevu," amesema Omar.

Naye Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Wete, Suleiman Ali Hamad, amewakumbusha wavuvi na wananchi kwa ujumla umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uvuvi, ikiwemo kukata leseni za uvuvi na kutumia vifaa vinavyokubalika kisheria.

Amesema kufuata sheria kutasaidia kupunguza migogoro, kulinda rasilimali za bahari na kuhakikisha shughuli za uvuvi zinaendelea kwa njia endelevu.

Kwa upande wao, Masheha walioshiriki mkutano huo wameahidi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao kuhusu madhara ya uvuvi haramu na umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya bahari.

Msheha wa Fundo, Khamis Abeid Salim, amesema ipo haja ya kuhamasisha matumizi ya mitego rafiki kwa mazingira ambayo hata inapopotea baharini haiendelei kuua samaki na viumbe wengine kwa muda mrefu.



Naye mkongwe wa uvuvi kutoka Ukunjwi, Kasanje Khamis, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya jamii, viongozi wa maeneo na mamlaka za uvuvi ni nguzo muhimu katika kutokomeza uvuvi haramu na kulinda rasilimali za bahari.

Washiriki wa mkutano huo wamekubaliana kuwa uhifadhi wa mazingira ya bahari ni jukumu la kila mwananchi, na kwamba usimamizi bora wa rasilimali hizo utachangia kuimarisha uchumi wa jamii zinazotegemea uvuvi pamoja na kuhifadhi bioanuwai ya bahari kwa vizazi vijavyo.


No comments