Breaking News

VITENDO VYA UTELEKEZWAJI WA WANAWAKE NA WATOTO BADO NIKILIO KWA WAKAAZI WA MAHONDA



Na Siti Ali.

Shehia ya Mahonda inapatikana Wilaya ya Kaskazini B, Unguja, ni eneo linalosifika kwa shughuli za kilimo, hasa uzalishaji wa miwa, na mwingiliano mkubwa wa kijamii. Hata hivyo, nyuma ya harakati hizi za kiuchumi, kuna changamoto nzito ya kijamii inayozidi kutishia mustakabali wa kizazi kijacho, tatizo sugu la utekelezaji wa watoto.

Ingawa Mahonda ni ukanda wa kilimo, kipato cha familia nyingi bado ni cha chini na cha msimu. Ugumu wa maisha huwapelekea baadhi ya wazazi (hasa akina baba) kukimbilia maeneo ya mijini au kwenye maeneo ya utalii kama Nungwi au Kendwa kutafuta maisha, na mwisho wake kusahau kutuma matunzo kwa familia zao walizoziacha nyuma.

Utekelezaji wa watoto, iwe ni kuacha kuwapatia chakula, elimu, matibabu au kuwatelekeza kabisa bila kujali usalama wao, unachochewa na mambo kadhaa maalumu ndani ya jamii.

Licha ya juhudi mbalimbali za Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali visiwani Zanzibar kupiga vita udhalilishaji na utekelezaji wa watoto kwa wakazi wa Mahonda, jambo hili bado ni donda ndugu linalohitaji uvumbuzi wa haraka.

Tatizo la migogoro ya talaka ni miongoni mwa mambo yanayochangia kesi nyingi za udhalilishaji ambazo zinarudisha nyuma ustawi wa jamii na kupelekea kupatikana kwa kizazi kisicho na maadili na kukosa utawala bora, kama takwimu za Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kiongwe chini ya Hakimu Luciano Makoenyengo zinavyoonesha.

"Takwimu kupitia Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kiongwe chini ya Hakimu Luciano Makoenyengo zinaonesha kuwa kwa mwaka 2025, jumla ya kesi 31 za udhalilishaji zimeripotiwa ambapo 25 zimeachiwa huru, 6 zinaendelea, watu 7 wamefungwa, 3 wametozwa faini, 14 wako huru na kesi 1 imeondolewa kutokana na mashahidi kutokufika mahakamani kwa muda mrefu.

Kwa mwaka 2026 kuanzia mwezi Januari hadi Mei, jumla ya kesi 14 za udhalilishaji zimeripotiwa ambapo kesi 4 zimemalizika, 10 zinaendelea, mtuhumiwa 1 ametozwa faini, 1 amefariki dunia, na kesi 2 zimeondoshwa kutokana na mashahidi kutokufika mahakamani kwa muda mrefu," ameeleza Hakimu Luciano.



Mkurugenzi wa Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini B, Shaaban Sariboko Makarani, amesema kuwa moja ya kazi wanazozifanya ni kutatua migogoro ya kisheria, ikiwemo ya utekelezaji wa watoto unaotokana na wimbi la talaka na kuvunjika kwa ndoa kwa muda mfupi, jambo ambalo halileti mustakabali mzuri wa utawala bora.

"Kama ilivyo katika maeneo mengi ya vijijini Unguja, kasi ya kuvunjika kwa ndoa huku Mahonda ni kubwa. Ndoa inapovunjika mara nyingi hakuna utaratibu rasmi wa kisheria unaofuatwa kuhakikisha watoto wanatunzwa. Wanaume wengi huacha majukumu yote ya malezi kwa wanawake ambao mara nyingi hawana vyanzo thabiti vya mapato," amesema Sariboko.

Sheha wa Shehia ya Mahonda, Ali Issa Kinoleni, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa mwingiliano wa kijamii unaotokana na harakati za kibiashara Mahonda huchochea vishawishi kwa vijana. Wasichana wengi wadogo huingia kwenye mahusiano yanayopelekea mimba zisizotarajiwa, jambo ambalo huathiri hali ya uchumi na ustawi wa jamii.

"Vijana wa kiume wanaowazalisha wasichana hawa mara nyingi hukimbia majukumu kwa hofu ya kukamatwa au kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha, hivyo kumwacha mtoto changa mikononi mwa mama ambaye naye bado ni mtoto kiumri," ameeleza Sheha huyo.

Mkazi wa Shehia ya Mahonda, Khadija Ali Mohammed, ameelezea athari za utekelezaji wa watoto katika maisha ya kila siku ya jamii.

"Matokeo ya kutelekezwa kwa watoto yanadhihirika wazi katika maisha yetu ya kila siku kwani hupelekea kuongezeka kwa utoro shuleni. Watoto wengi wanaokosa matunzo hulazimika kuacha shule ili kufanya vibarua mashambani au kuuza bidhaa ndogo ndogo ili kusaidia kupata chakula cha familia," amesema Khadija.

Suala la malezi linahitaji ushirikiano wa wazazi wote wawili. Ushirikiano huo unapokosekana hutokea madhara makubwa kwa watoto, ikiwa ni pamoja na kukosa usimamizi na kupelekea kuporomoka kwa maadili na kuongezeka kwa vitendo viovu, kama anavyoeleza Sheikh na Imamu wa Shehia ya Mahonda, Salum Gharib Salum.

"Kumekuwa na mmomonyoko wa maadili na kuibuka kwa makundi hatari yanayotokana na ukosefu wa usimamizi wa wazazi, jambo linalowapelekea watoto kujiingiza katika makundi ya kihalifu, matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya wizi vinavyovuruga amani ya shehia na nchi kwa ujumla," amesema Sheikh Salum.



Mchungaji wa Shehia ya Kitope, Emmanuel Malingila, amesema kuwa kupitia mafunzo waliyoyapata kutoka Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya utekelezaji wa watoto pamoja na udhalilishaji.

"Madhara mengi hujitokeza watoto wanapotelekezwa, ikiwemo udhalilishaji wa kingono. Watoto wanaotelekezwa huwa katika hatari kubwa ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kingono kwa sababu hukosa kinga na uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi wao," amesema Mchungaji Emmanuel.

Wadau na wahisani mbalimbali wanaosaidia jamii, wakiwemo Idara ya Maendeleo ya Kanisa Katoliki Zanzibar kupitia mradi wa uwezeshaji wa haki za binadamu na utawala bora kwa ufadhili wa Misereor, wamekuwa wakichukua jitihada mbalimbali katika kulikemea tatizo hilo kwa kutoa elimu kwa jamii na wadau kuhusu haki na wajibu wa kila mmoja.

Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Msafiri Thomas Mombo, amesema:

"Sisi Kanisa Katoliki tunachukua juhudi mbalimbali kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi. Tunahimiza jamii kushirikiana kuondoa tatizo hili kwa kuimarisha elimu ya sheria kupitia wasaidizi wa sheria (Paralegals) katika Wilaya ya Kaskazini B, pamoja na kutoa elimu ya ndoa kwa wanajamii ili kupunguza migogoro ya kifamilia na kuhakikisha familia zinapata haki zao."

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Zanzibar, Siti Abbas Ali, amesema kuwa idara hiyo imekuwa ikipokea kesi nyingi za utekelezaji wa watoto na kuiomba jamii kuitumia kikamilifu Sheria ya Mtoto ya Zanzibar (Na. 6 ya mwaka 2011) katika kulinda haki za watoto.

"Tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali ikiwemo kampeni endelevu za kuielimisha jamii ya Mahonda kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango, madhara ya ndoa za mapema na wajibu wa kidini na kijamii wa kulea watoto. Pia kuna programu maalumu za mikopo na mafunzo ya ujasiriamali kwa akina mama walioachiwa watoto ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi waweze kuwalisha na kuwasomesha watoto wao hata wanapotelekezwa na waume zao," amesema Siti.

Watoto ndio nguvu kazi na viongozi wa kesho wa Shehia na taifa kwa ujumla. Utekelezaji wao ni bomu la kijamii linalosubiri kuripuka ikiwa halitashughulikiwa sasa. Ni wajibu wa kila mkazi wa Mahonda kubadili mtazamo na kuelewa kuwa kulea mtoto si jukumu la mama pekee au Serikali, bali ni wajibu wa pamoja wa kulinda utu na mustakabali wa jamii yetu.


No comments