WATAALAMU UFUGAJI SAMAKI MKOMBOZI KWA WAJASIRIAMALI WA SAMAKI WA MAJI BARIDI.
Na Said Khamis
Ufugaji wa Samaki ni ajira kwa vijana na Taifa kwa ujumla hivyo hakuna budi Serikali kuunga mkono shughuli za ufugaji wa samaki wa maji baridi nchini.
Hayo ameyasema Mkuu wa Kikundi cha Rwambo Mohammed Salim Othman Mfugaji wa Samaki wa maji baridi baada ya kutembelewa na Wataalamu wa ufugaji wa viumbe maji huko Kwarara Wilaya ya Magharibi "B".
Amesema ufugaji wa samaki aina ya Sato unaleta faida kubwa kibiashara kwa Soko la ndani hususani kipindi cha kusimama kwa bamvua baharini jambo ambalo huleta changamoto ya uhaba wa samaki hapa nchini.
Pia Othamn ameiomba Serikali kuendelea kuwaletea Wataalamu ili kuwatatulia changamoto wanazokumbanazo katika ufugaji ikiwemo utengezaji wa chakula cha Samaki ili kupunguza gharama za ufugaji huo.
Nao Wataalamu kutoka Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini Zanzibar Afisa Thomas Raphiel na Afisa Hassan Fumu Mabrouk wamekiomba kikundi cha Rwambo kufuga vifaranga vya saizi moja na aina moja ili kupata Samaki wakubwa ambao wataleta tija katika biashara.
Aidha wamesema upo uwezekano wa kutia Kambare wadogo kwenye bwawa la Samaki wa Sato ili kupunguza vifaranga vya Sato kuzaliana kwa wingi nakupelekea idadi kubwa ya Samaki bila ya mpangilio.
Kikundi cha Rwambo kina jumla ya wanachama 5 na kimeajiri mfanyakazi mmoja kwa ajili ya ulinzi kwenye eneo hilo na kikundi hicho kimeanza ufugaji huo Septemba 2025.



No comments