Breaking News

MAFUNZO YA UANDISHI WA KISAYANSI, UCHAPISHAJI NA UANDAAJI WA SERA YATOA MWANGA KWA WATAFITI.

Na Said Khamis

‎Vijana wametakiwa kujifunza mbinu za kisasa za uandishi na uchapishaji wa kazi za tafiti ili kuongeza ubora wa kazi zao na kuzifanya zitambulike.

‎Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Baharini Zanzibar ZAFIRI Ali Said Ali wakati akifungua mafunzo ya uandishi wa kisayansi, uchapishaji pamoja na uandaaji wa sera huko Maruhubi wilaya ya Mjini.

‎Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watafiti,vijana na wadau mbalimbali katika kuandika na kuwasilisha tafiti kwa njia ya kitaalamu zaidi.



‎Ameeleza kuwa uandishi wa kisayansi ni nyenzo muhimu katika kuendeleza tafiti na kusaidia utoaji wa maamuzi sahihi katika jamii na taasisi mbalimbali hivyo ipo haja kwa vijana kujifunza mbinu za kisasa za uandishi na uchapishaji wa kazi za tafiti ili kuongeza ubora wa kazi zao.

‎Kwa upande wake Remmy Lema ambaye ni Afisa Mwandamizi kutoka  Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia Duniani IUCN amesema mafunzo hayo ni moja wapo ya mkakati chini ya mradi huo wa kuzijengea uwezo taasisi mbalimbali zinalizojikita kwenye tafiti za ekolojia ya bahari na misitu ya ukanda wa pwani ikiwemo ZAFIRI. 


‎Aliendelea kusema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wataalamu na watafiti  katika ukusanyaji na uchakataji wa  taarifa  ili waweze kutoa mashapisho mbalimbali ya kisayansi mbali na kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar namna ya kuboresha usimamizi wa ikolojia ya bahari Zanzibar

‎Nae mtalamu kutoka chuo Kikuu cha Dar-es-Salam Prof. Samuel Mchele Limbu amesema  mafunzo hayo yamekuja muda muwafaka na ni muhimu  hasa kwa vijana wanaoanza kazi sasa kupatiwa taaluma hio ambayo itaweza kuwasaidia kuandika kisayansi na uandaaji mzuri wa miandiko ya kisera ambayo yatayowashawishi watunga sera kuweza kutumia matokeo ya tafiti wanazozifanya.



‎‎Hata hivyo Prof.Limbu ametoa wito kwa vijana kutumia fursa hiyo kujifunza  kuhusu tafiti, uchambuzi wa taarifa na namna ya kuandika ushauri wa kisera zitakazoweza kusaidia na kuleta mabadiliko yakuendeleza taifa  kwa kufanya tafiti zinazoendana na mahitaji ya kisera na mipango ya muda mrefu ili kuweza kusaidia jamii.



‎Mafunzo hayo yameratibiwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia Duniani (IUCN) kupitia Mradi wa Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu unaofadhiliwa na Ubalozi wa Umoja wa Ulaya Tanzania, na takribani watafiti 30 wamepatiwa mafunzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku 6 huko ZAFIRI Maruhubi Zanzibar.‎


No comments