Breaking News

WANANCHI BAMBI WALIA, UBOVU WA BARABARA, MBELE YA MKUU WA WILAYA



Na Fatma Rajab.

Wananchi wa Shehia ya Bambi, Wilaya ya Kati Unguja, wameeleza kilio chao juu ya changamoto za barabara mbovu, migogoro ya ardhi, uhaba wa maji safi na huduma duni za afya, wakiiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuchukua hatua za haraka kuzipatia ufumbuzi.

Malalamiko hayo yalitolewa katika kikao cha kusikiliza kero za wananchi kilichofanyika katika viwanja vya Skuli ya Maandalizi Bambi, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kati, Rajab Ali Rajab, alifika kusikiliza matatizo ya wananchi na kutafuta njia za kuyatatua.

Wananchi hao walisema changamoto hizo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa muda mrefu licha ya juhudi wanazofanya kujiletea maendeleo.

Akizungumza katika kikao hicho, Haji Juma Haji alisema tatizo kubwa ni ubovu wa barabara kutoka Bambi hadi Uzi pamoja na kukosekana kwa njia zinazounganisha mashamba na barabara kuu.

Alisema hali hiyo imekuwa ikiwapa ugumu wakulima kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda sokoni, jambo linalosababisha kushuka kwa kipato cha wananchi wanaotegemea kilimo.

“Tunazalisha mazao mengi lakini tunapata shida kuyafikisha sokoni kutokana na ubovu wa barabara na njia za mashambani,” alisema Haji.

Mbali na changamoto ya barabara, wananchi pia walilalamikia mgogoro wa ardhi kati yao na Kikosi cha Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU), wakisema mgogoro huo umeendelea kwa muda mrefu bila kupatiwa suluhisho la kudumu.

Ahmed Mrisho alisema baadhi ya wawekezaji wamepewa maeneo makubwa ya ardhi huku wananchi wa eneo hilo wakikosa manufaa ya moja kwa moja kutokana na uwekezaji huo.

Alisema hali hiyo imewaacha wananchi wengi bila maeneo ya kilimo licha ya kutegemea sekta hiyo kama chanzo kikuu cha kipato.

“Wananchi wengi hawana tena ardhi ya kulima kwa sababu maeneo mengi yamechukuliwa na wawekezaji,” alisema Ahmed.

Wananchi hao pia walieleza tatizo la maji safi na salama, wakisema wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.

Kwa upande wake, Mwaka Khamis Maneno aliiomba Serikali kuboresha huduma za afya katika kituo cha afya cha Bambi kwa kurejesha vifaa vya uzazi.

Alisema ukosefu wa vifaa hivyo unawalazimu wajawazito kwenda kutafuta huduma katika maeneo ya mbali hali inayohatarisha afya zao.

Naye Yahya Mohammed Amani alisema vijana wengi wanahitaji maeneo ya misitu kwa ajili ya kuanzisha miradi ya ufugaji wa nyuki lakini wanakosa maeneo na mitaji ya kuwawezesha kujiajiri.

Aidha, wananchi hao waliomba kupatiwa elimu ya namna ya kuandika miradi ili waweze kupata mikopo inayotolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kati Unguja, Mwanaisha Ali Said, alisema Serikali imeweka mikopo maalumu kwa ajili ya makundi hayo lakini wananchi wengi bado hawajaitumia vizuri kutokana na kutokuwa na vikundi rasmi.

Alisema hadi sasa vikundi 44 pamoja na watu wenye ulemavu 15 tayari wamepatiwa mikopo ndani ya wilaya hiyo.



Naye Mkuu wa Wilaya ya Kati, Rajab Ali Rajab, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itazifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa hatua kwa hatua.

Alisema Serikali ina mpango wa kujenga barabara za eneo hilo kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Rajab alisema ataendelea kufanya ziara katika shehia zote 42 za Wilaya ya Kati kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.


No comments