Breaking News

WAJASIRIAMALI WALIA NA OCCUPATION HEALTH UNITY KUHUSU VIPIMO VYA TYPHOID

Na Mwandishi wetu.


Na Maryam Nassor

WAJASIRIAMALI nchini wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuifuatilia kwa karibu Hospitali ya Occupation Health Unity iliyopo Mazizini, kufuatia malalamiko kuhusu huduma za vipimo vya afya vinavyotolewa, kuwa na wasiwasi , hususan  vipimo vya ugonjwa wa Typhoid.

Wakizungumza na waandishi wa habari huko Magomeni Jitini Unguja, baadhi ya wajasiriamali walidai kuwa majibu ya vipimo wanavyopewa hospitalini hapo hutofautiana na yale wanayopata katika hospitali nyengine.

Mjasiriamali Maryam Ali Mussa, alisema alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kupima afya ili aweze kuwasilisha cheti katika Baraza la Manispaa kwa ajili ya kupata kitambulisho cha ujasiriamali.

Alisema, baada ya kujitambulisha kuwa ni mjasiriamali wa kuuza supu, aliambiwa alipe shilingi 53,000 kwa ajili ya vipimo vya magonjwa manne ikiwemo homa ya ini A na B, mkojo pamoja na Typhoid.

Maryam alisema  kuwa, baada ya vipimo hivyo alielekezwa kurejea nyumbani huku majibu yakitumwa kupitia simu yake ya mkononi.

“Nilitumiwa majibu kwenye simu na kwenye cheti hicho kuliandikwa ‘Positive’. Sikufahamu maana yake, lakini baada ya kuona hivyo nilipatwa na mshtuko na kuzimia kwa sababu nilipima magonywa manne nikihofia yote ninayo , na nilipopata fahamu nilijikuta nipo Hospitali ya Mafunzo ya Kilimani,” alisema Maryam.

Alisema  kuwa ,alipofikishwa Hospitali ya Mafunzo wazazi wake  walisema afanyiwa vipimo tena na majibu yalionesha kuwa hakuwa na ugonjwa wowote.

Alieleza kuwa , yeye pamoja na ndugu zake walirejea tena katika Hospitali ya Occupation Health Unity kuuliza sababu ya tofauti ya majibu hayo.

Aidha alisema  kuwa ,mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo alimueleza kuwa vipimo vyao vilionesha ana Typhoid, hivyo alitakiwa kutumia dawa kwa muda wa siku 14 na kurejea tena kupima kwa gharama ya shilingi 15,000 ili aweze kupatiwa cheti cha kuwasilisha halmashauri kwa ajili ya kupata kitambulisho cha ujasiriamali.

Naye mzazi wa mjasiriamali huyo, Amana Suleiman, alisema ni vyema Serikali ikaingilia kati suala hilo kwani wana hofu kuwa baadhi ya wagonjwa wanaandikiwa kuwa na maradhi ili warejee tena hospitalini hapo kwa ajili ya vipimo vingine na kuongeza gharama hawana hayo maradhi.

Alisema  kuwa ,wajasiriamali wengi wanaokwenda kupima katika hospitali hiyo huambiwa wana Typhoid, lakini wanapopima katika hospitali nyingine hukutwa hawana maradhi hayo.

“Tunaiomba Serikali yetu sikivu ilifuatilie suala hili ili kupata ufumbuzi, kwani tunahisi baadhi ya watoa huduma katika hospitali hiyo hawafuatii maadili ya taaluma zao,” alisema Amana.

Naye Farid Jabir Mjasiriamali wa Chakula, alisema alienda kupima kituo hicho maarufu kama Kituo cha Covid akaandikiwa kuwa ana ugonywa wa Typhoid lakini hakutumia dawa yoyote, aliporudi mara ya pili kupima akaambiwa amepona na hana ugonywa huo.

" Mimi niliporudi mara ya pili kupima baada ya siku 14 nililipa elfu 15,000 na kufanya vipimo nikaonekana nimepona Typhoid lakini cha kushangaa sikuwahi kutumia dawa nilizoandikiwa nikanunuwe nikaonekana nimepona hapo ndipo nikaanza kutilia wasi wasi kituo hichi" anasema Farid.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa kutoka Hospitali ya Occupation Health Unity, Zainab Abubakar, alisema ni kweli wakati mwingine hutokea tofauti ya majibu kati ya hospitali hiyo na hospitali nyingine.

“Ni kweli huwa tunapokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wateja wetu wanaokuja kufanya vipimo kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali. Wakati mwingine hupima hapa na kuonekana wana maradhi, lakini wanapokwenda hospitali nyingine hukutwa hawana,” alisema Zainab.


No comments