JIFUNZENI WELEDI KUPITIA WALIOFANIKIWA.
Na Siti Ali
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar, ndugu Shaib Ibrahim, amewataka viongozi wa Mabaraza ya Vijana ngazi ya Shehia kuwa tayari muda wote kujifunza ili waweze kuwaongoza vijana wenzao kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya jamii zao. Amesema viongozi wenye maarifa na uelewa mpana ndio msingi wa kuibua vijana wenye maadili, uwezo na mchango chanya katika jamii.
Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa Wenyeviti, Makatibu na Makamo Wenyeviti wa Shehia nane za Wilaya ya Kaskazini A yaliyoandaliwa na ZAFAYCO na kufanyika Ukumbi wa Michenzani Mall. Amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuwawezesha viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Aidha, amesisitiza kuwa Sera ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar ya mwaka 2023 imeainisha maeneo 14 muhimu yanayowahusu vijana, yakiwemo ajira, afya, mazingira, ushiriki na ushirikishwaji. Ameeleza kuwa viongozi wa vijana wanapaswa kuyaelewa kwa kina maeneo hayo kwa kuwa ndio msingi wa ustawi na maendeleo ya vijana Zanzibar.
Akizungumzia suala la ushiriki na ushirikishwaji, ndugu Shaib amesema vijana wanapaswa kuwa na ushiriki wenye tija katika shughuli za maendeleo badala ya kushiriki kwa mazoea.
Amesema vijana wanahitaji kutumia nafasi walizonazo kutoa mawazo, kushiriki katika maamuzi na kuchangia maendeleo ya maeneo yao kwa vitendo.
Sambamba na hilo, ameupongeza uongozi wa ZAFAYCO kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji katika kutatua changamoto zinazowakabili vijana. Pia ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi za Baraza la Vijana Zanzibar ili liweze kufikia malengo yake ya kuwawezesha vijana.
Akizungumza kwa niaba ya ZAFAYCO, Mkuu wa Programu Asya Said Mohamed amesema kupitia mradi wa “Wajibu Wako, Haki Yetu”. vijana wengi wamewezeshwa kufahamu wajibu wao pamoja na kuwa na uthubutu wa kuwasilisha changamoto zao kwa viongozi wa maeneo yao.
Ameongeza kuwa programu ndogo ya Civic Trio inalenga kuimarisha utendaji kazi wa Mabaraza ya Vijana Zanzibar ili yafanye kazi kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan, akiwasilisha mada ya uongozi na uelewa wa Baraza hilo, amewataka viongozi hao kuwa sehemu ya mabadiliko ya kiutendaji katika Shehia zao.
Amesema uchaguzi umekwisha na sasa vijana wanawategemea viongozi hao katika kusimamia maendeleo na kuwahamasisha vijana kujiunga na Baraza hilo ambalo ni jukwaa muhimu kwao.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza kupatiwa elimu hiyo wakisema itawasaidia katika utendaji wao wa kila siku. Pia wameiomba ZAFAYCO kuendelea kutoa mafunzo kama hayo kwa viongozi wa vijana kadri hali itakavyoruhusu.
Mafunzo hayo ya siku moja yaliwashirikisha viongozi kutoka Shehia za Kidombo, Mkwajuni, Kivunge, Gamba, Chaani, Pwani Mchangani, Moga na Mto wa Pwani.
.jpeg)



No comments