ZANZIBAR ITAENDELEA KUIMARISHA UTAWALA BORA AFRIKA MASHARIKI.
Na Siti Ali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameihakikishia Jumuiya ya Mawakili ya Afrika Mashariki ushirikiano wa kina katika kuimarisha utawala wa sheria na ushirikiano wa kikanda katika nchi za Afrika Mashariki. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na jopo la mawakili wa Jumuiya hiyo wakiongozwa na Rais wa Jumuiya hiyo, Ndg. Ramadhan Aboubakar, waliofika Ikulu Zanzibar kujitambulisha.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania ikiwemo Zanzibar itaendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha umoja wa Afrika Mashariki kiuchumi, kijamii na kidiplomasia. Amepongeza hatua ya Jumuiya hiyo kufanya Mkutano Mkuu wa mwaka Zanzibar mwezi Novemba 2026, akieleza kuwa utasaidia kuwakutanisha mawakili wa Afrika Mashariki pamoja na kufungua fursa za kiuchumi na uwekezaji, huku akiihakikishia Jumuiya hiyo ushirikiano mkubwa katika kufanikisha mkutano huo.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya utalii kwa kuimarisha utalii wa mikutano ya kimataifa. Naye Rais wa Jumuiya ya Mawakili ya Afrika Mashariki, Wakili Ramadhan Aboubakar, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa maendeleo makubwa ya miundombinu na hali ya amani na utulivu inayoendelea kushuhudiwa Zanzibar chini ya uongozi wake.



No comments