Breaking News

WADAU WATAKIWA KUTOA MAONI KUIMARISHA MPANGO WA MATUMIZI YA BAHARI KWA USAWA WA KIJINSIA





Na Said Khamis.

Wadau wa sekta ya bahari wametakiwa kutoa maoni yao yatakayosaidia kuandaa mpango madhubuti wa utekelezaji wa shughuli za kiuchumi zitokanazo na rasilimali za bahari, huku wakihimiza kuzingatiwa kwa usawa wa kijinsia katika matumizi ya rasilimali hizo.

Akifungua warsha ya siku moja ya Mpango wa Utekelezaji wa Marine Spatial Planning (MSP) kuhusu ujumuishaji wa kijinsia katika matumizi ya bahari, iliyofanyika katika Ukumbi wa Marumaru, Wilaya ya Mjini, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo na Uratibu wa Uchumi wa Buluu, Mondy Christopher Mohando, amesema usawa wa kijinsia ni jambo la msingi katika kufanikisha maendeleo ya sekta ya bahari.



Amesisitiza kuwa wadau wa masuala ya bahari wanapaswa kulitazama kwa karibu suala hilo ili kuhakikisha kunakuwepo na mafanikio ya pamoja yanayojumuisha makundi yote katika jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Usimamizi wa Bahari kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu, Hamida Abdulla Mohamed, amesema lengo la warsha hiyo ni kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali yatakayosaidia katika utekelezaji bora wa mpango wa matumizi ya bahari, huku yakihakikisha kuwa usawa wa kijinsia unazingatiwa kikamilifu.



Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira, Lucy Magembe, amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa kijinsia, akieleza kuwa taifa lina idadi kubwa ya vijana, hususan vijana chipukizi, wanaoshiriki katika shughuli za maendeleo na hivyo wanahitaji kupewa nafasi sawa katika kunufaika na rasilimali za bahari.



Aidha, amesema mpango huo unalenga kuhakikisha ushirikishwaji jumuishi, kuondoa vikwazo vya kijinsia, na kukuza maendeleo endelevu katika sekta ya bahari. Hatua hiyo pia inatarajiwa kuboresha usawa katika maamuzi yanayohusu fursa za kiuchumi zitokanazo na rasilimali za bahari nchini.



No comments