Breaking News

KESI 157 ZA UDHALILISHAJI ZAFIKISHWA MAHAKAMANI MJINI MAGHARIBI.

 


Na Said Khamis.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limeeleza kuwa jumla ya kesi 157 za udhalilishaji zimefikishwa mahakamani katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zake zilizopo Madema, Mjini Unguja, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, SACP Richard Tadei Mchomvu, amesema hatua hiyo inaonesha jitihada zinazoendelea za kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji katika jamii.

Kwa mujibu wa Kamanda Mchomvu,  Wilaya ya Magharibi A inaongoza kwa kuwa na kesi 61 za udhalilishaji, ikifuatiwa na  Wilaya ya Magharibi B ikiwa na kesi 54, huku Wilaya ya Mjini ikiwa na kesi 42 ambapo kesi zote tayari zipo katika hatua mbalimbali za mahakamani.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza mahakamani kutoa ushahidi ili kuhakikisha watuhumiwa wa vitendo hivyo wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.

Katika hatua nyingine, akizungumzia hali ya usalama kwa mwezi Februari, Kamanda Mchomvu amesema Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata mali mbalimbali zilizoibiwa, zikiwemo pikipiki, mapanga, televisheni, nondo za milimita 16 pamoja na simu tano. Aidha, watuhumiwa sita wa wizi wa mifugo wamekamatwa.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana nalo kwa kutoa taarifa za vitendo vya kihalifu pamoja na wahalifu waliopo katika maeneo yao ili kudumisha usalama na amani nchini.


No comments