ZIDO YAKABIDHI VIFAA VYA KILIMO CHA MWANI KWA WANAWAKE UNGUJA
Taasisi zisizo za kiserikali zimeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi, hususan wanawake, kupitia miradi mbalimbali ya kuwawezesha kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Hali hiyo imejidhihirisha baada ya Taasisi ya Zanzibar International Development Organisation (ZIDO) kukabidhi vifaa vya kilimo cha mwani kwa wakulima wanawake katika shehia za Bungi na Kikungwi, Wilaya ya Kati Unguja.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa ZIDO, Makame Ramadhan Mbanja, alisema msaada huo unalenga kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ufanisi kwa wakulima hao.
Alieleza kuwa wanawake wengi wanaojishughulisha na kilimo cha mwani hukabiliwa na changamoto za ukosefu wa mitaji na vifaa, hali inayodumaza jitihada zao za kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wao, wakulima walionufaika na msaada huo walieleza furaha yao, wakisema utawasaidia kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato, huku wakitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia sekta hiyo.
Jumla ya wakulima 100 wamenufaika na msaada huo uliogharimu shilingi milioni 13, ambapo vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kamba na taitai kwa ajili ya kuimarisha kilimo cha mwani
Reviewed by ZANNEWS UPDATE
on
April 27, 2026
Rating: 5


No comments