Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) umezipeleka mahakamani taasisi tatu za binafsi kwa tuhuma za kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati pamoja na kutowasajili wafanyakazi wao katika mfuko huo.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya taasisi hizo kubainika kukiuka taratibu na masharti ya mfuko huo, hali ambayo imeelezwa kuwa inahatarisha ustawi wa wafanyakazi na haki zao za msingi.
Akizungumza mara baada ya kusomwa kwa mashitaka hayo mahakamani, mwanasheria wa ZSSF, Ramadhan Juma Suleiman, alisema uamuzi wa kuzipeleka taasisi hizo mahakamani umetokana na kukiuka sheria za mfuko huo.
Alieleza kuwa mbali na kushindwa kuwasilisha michango kwa wakati, taasisi hizo pia zimeshindwa kuwasajili wafanyakazi wao katika mfuko huo, jambo ambalo ni la lazima kisheria.
Mashitaka hayo yalisomwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mazizini, Abubakar Suleiman Thabit, ambaye alisikiliza maelezo ya upande wa mashtaka dhidi ya taasisi hizo.
Akizitaja taasisi zinazokabiliwa na mashitaka, Suleiman alisema ni pamoja na EDST Hospitali iliyopo Saateni, ambayo inadaiwa kushindwa kuwasajili wafanyakazi 300 pamoja na kutowasilisha michango yao ZSSF.
Kwa mujibu wa maelezo yake, hospitali hiyo haijawasilisha michango kuanzia Mei 2024 hadi mwaka huu, huku jumla ya shilingi bilioni 1,771,526,112 zikidaiwa kutolipwa.
Akiitaja Taasisi nyingine kuwa ni Horizon Zanzibar Limited, ambayo mwajiri wake anadaiwa kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi ndani ya muda uliowekwa kisheria.
AIisema kampuni hiyo haikuwasilisha michango kuanzia Septemba 2024 hadi Desemba 2025, ambapo kiasi cha shilingi 13,325,550 hakijalipwa.
Aidha, kampuni nyengine alisema Exatic Tour Safari Limited nayo inakabiliwa na mashitaka ya aina hiyo baada ya kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wake.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, kampuni hiyo haijawasilisha michango kuanzia Agosti 2024 hadi Desemba 2024, ambapo jumla ya shilingi milioni 91,366,368 hazijawasilishwa.
Alisema kwa mujibu wa kisheria, kosa la kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi ni kinyume na kifungu cha 17(3) na 4(a)(b) cha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar namba 2 ya mwaka 2005, kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.
Aidha, kanuni ya 56(1)(d) na (2) ya kanuni za mwaka 2007 pia inasisitiza wajibu wa waajiri kuwasilisha michango hiyo kwa wakati.
Vilevile, kushindwa kuwasajili wafanyakazi ni kosa chini ya kifungu cha 18 cha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ya mwaka 2005.
Mwanasheria huyo alisisitiza kuwa vitendo hivyo vinakiuka sheria za mfuko wa hifadhi ya jamii na kuwanyima wafanyakazi haki zao muhimu za kijamii na kiuchumi.
Alizitaka taasisi zote kuhakikisha zinawasilisha michango kwa wakati na kuwasajili wafanyakazi wao ili kuepuka hatua za kisheria.
“ZSSF kwa sasa haitaivumilia taasisi yoyote itakayokiuka sheria hizi; hatua kali za kisheria zitachukuliwa bila kusita,” alisema.
Aliongeza kuwa mfuko huo umejipanga kuhakikisha unalinda mustakabali wa wafanyakazi kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria.
Kwa upande wake, Hakimu Abubakar Suleiman Thabit alitoa hati ya kukamatwa kwa watuhumiwa waliotajwa ili wafikishwe mahakamani.
Alisema watuhumiwa hao wanatakiwa kufikishwa mahakamani Mei 19 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa kesi zao.
ZSSF imeeleza kuwa itaendelea kuchukua hatua dhidi ya waajiri wote watakaokiuka sheria ili kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa kikamilifu.

No comments