SERIKALI YASISITIZA KIPAUMBELE CHA HUDUMA KWA WATOTO WENYE TAWAHUDI ZANZIBAR
Na Said Khamis
WIZARA ya Afya Zanzibar imeweka msisitizo mkubwa katika kushughulikia suala la tawahudi (usonji) kama sehemu ya ajenda muhimu ya afya ya akili na maendeleo ya mtoto, kwa lengo la kuhakikisha watoto wenye hali hiyo wanapata huduma stahiki mapema na kwa ufanisi. Kauli hiyo ilitolewa katika kongamano la maadhimisho ya Siku ya Tawahudi Duniani lililofanyika katika ukumbi wa Shekh Idrisa Abdulwakili, Kikwajuni Unguja, likiwakutanisha wadau wa sekta za afya, elimu na ustawi wa jamii ili kuongeza uelewa na kusogeza huduma karibu zaidi kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mngereza Mzee Miraji, alisema serikali inatambua umuhimu wa kushughulikia changamoto za tawahudi kwa mtazamo mpana wa kisera. Alieleza kuwa juhudi hizo zinahusisha uwekaji wa mikakati madhubuti inayotegemea ushahidi wa kitaalamu pamoja na ushirikishwaji wa sekta mbalimbali ili kuhakikisha huduma zinawafikia wahitaji kwa wakati.
Miraji alibainisha kuwa serikali tayari imeanza kuimarisha huduma za afya ya mtoto katika ngazi ya msingi, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa mapema wa dalili za tawahudi. Aidha, alisema huduma za tiba ya usemi na tiba ya viungo zinaendelea kuingizwa katika mfumo wa afya ili kuwasaidia watoto wenye changamoto za maendeleo ya mawasiliano na mwili.
Katika kongamano hilo, wataalamu wa afya waliwasilisha mada mbalimbali kuhusu tawahudi, zikigusia chanzo, dalili na njia za kusaidia watoto wenye hali hiyo. Daktari Bingwa wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Muhimbili, Dk. Leonida Isidory Ngongi, alieleza kuwa mtoto mwenye tawahudi anahitaji msaada maalum ili kufikia ukuaji bora.
Dk. Ngongi alisema tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watoto wanaweza kugundulika kuwa na tawahudi wakiwa chini ya umri wa miaka miwili. Aliongeza kuwa dalili za awali ni pamoja na changamoto za mawasiliano, kuchelewa kuzungumza na matatizo katika ukuaji wa kimwili, kama kushindwa kushikilia kichwa mapema.
Aidha, alifahamisha kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, mtoto mmoja kati ya 100 duniani anaweza kuwa na tawahudi. Alieleza kuwa baadhi ya tafiti za Afrika zinaonesha kiwango cha asilimia 0.3 nchini Kenya na asilimia 2.3 nchini Nigeria, huku Tanzania ikiwa haina takwimu rasmi kutokana na changamoto ya uhifadhi wa taarifa.
Akizungumzia chanzo cha tawahudi, alisema bado hakuna sababu halisi iliyothibitishwa kisayansi, ingawa vinasaba vinatajwa kuwa miongoni mwa vihatarishi vikuu. Aliongeza kuwa uwezekano wa mapacha wote kuwa na hali hiyo huongezeka endapo mmoja atagundulika, huku baadhi ya magonjwa ya kurithi na lishe duni vikichangia hatari hiyo.
Kwa upande mwingine, wataalamu na wadau walisisitiza umuhimu wa familia, jamii na serikali kushirikiana katika kusaidia watoto wenye tawahudi. Wazazi walieleza changamoto za ukosefu wa huduma bora na mzigo wa malezi unaowaathiri kiuchumi, huku asasi za kiraia zikihimiza kuwepo kwa mkakati maalum wa kitaifa na kuboreshwa kwa miundombinu rafiki ili kuhakikisha watoto wenye usonji wanapata haki na kushiriki kikamilifu katika jamii bila ubaguzi.
Reviewed by ZANNEWS UPDATE
on
April 09, 2026
Rating: 5

No comments