MIRADI YA BILIONI 44.7 KUNUFAISHA WANANCHI WILAYA YA KATI KUPITIA MBIO ZA MWENGE WA UHURU
Na Fatma Rajab.
Jumla ya miradi mitano yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 44.7 inatarajiwa kukamilika na kuzinduliwa sambamba na kuwekewa mawe ya msingi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu katika Wilaya ya Kati.
Akizungumza katika kikao cha maandalizi kilichowakutanisha watendaji wa wilaya hiyo kilichofanyika Dunga, Mkuu wa Wilaya ya Kati, Rajab Ali Rajab, alisema maandalizi ya miradi hiyo yamekamilika kwa kiasi kikubwa na ipo tayari kwa ajili ya shughuli za Mwenge wa Uhuru.
Alieleza kuwa miradi hiyo inagusa sekta mbalimbali muhimu za kijamii ikiwemo afya, elimu, miundombinu ya barabara, uwekezaji pamoja na michezo, hatua inayolenga kuimarisha ustawi wa wananchi na kuongeza kasi ya maendeleo endelevu.
Aidha, alifafanua kuwa mbali na uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi hiyo, pia kutakuwa na shughuli mbalimbali za kijamii zitakazofanyika sambamba na mbio za Mwenge wa Uhuru.
Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na upandaji wa miti aina ya mikoko, huduma ya upimaji afya bure kwa wananchi, maonyesho ya wajasiriamali pamoja na kongamano la vijana litakalolenga kuhamasisha ushiriki wao katika maendeleo ya jamii.
Mkuu huyo wa wilaya aliwahimiza wananchi wa Wilaya ya Kati na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli hizo ili kuhakikisha mbio za Mwenge wa Uhuru zinafanikiwa na kuleta tija inayokusudiwa.
Katika hatua nyingine, alitaja miradi itakayopitiwa na Mwenge huo kuwa ni pamoja na mradi wa Kituo cha Afya Tunguu, Skuli ya Sekondari Koani, daraja la Unguja Ukuu-Uzi, pamoja na mradi wa viwanja vya michezo Unguja Ukuu Kaebona.
Aliongeza kuwa mradi wa Swahili Tent Village uliopo Kijundu utaekewa jiwe la msingi, huku mbio za Mwenge wa Uhuru zikitarajiwa kuanza rasmi Aprili 9 mwaka huu katika Wilaya ya Kati, baada ya kukamilika katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kukabidhiwa Mkoa wa Kusini Unguja, zikiwa na kauli mbiu isemayo, “Tanzania yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”



No comments