WALIMU IPA WATAKIWA KUJIFUNZA KWA HARAKA, KUENDANA NA TEKNOLOJIA.
Na Said Khamis.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo, amewataka walimu na wanafunzi wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) kujifunza kwa bidii na kujiendeleza ili kwenda sambamba na kasi ya matumizi ya sayansi na teknolojia duniani.
Balozi Kombo ameyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Mafunzo kwa Watumishi wa Umma (Chuo cha Utawala wa Umma IPA lililopo Tunguu, hafla iliyofanyika katika kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema kwa sasa dunia imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia inayorahisisha utekelezaji wa majukumu kwa weledi na ufanisi mkubwa, hivyo ni muhimu kwa walimu na wanafunzi kuwa tayari kujifunza zaidi ili kufanya kazi kwa utaalamu na kuepuka kubaki nyuma katika ushindani wa kimataifa.
“Hivi sasa ulimwengu umebadilika kwa kasi kupitia matumizi ya teknolojia. Ni wajibu wenu walimu na wanafunzi kujifunza kwa bidii ili kufanya kazi kwa utaalamu na kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia,” amesema Balozi Kombo.
Aidha, kutokana na kuthamini umuhimu wa elimu, Waziri Kombo ametangaza kutoa nafasi tano za ufadhili kwa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) kwa ajili ya kwenda kujifunza nje ya nchi, lengo likiwa ni kuongeza maarifa, ujuzi na upeo wa mawazo kwa wanufaika wa chuo hicho
Ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kudumisha na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa maslahi mapana ya taifa
Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi wa Umma, Mhe. Haroun Ali Suleiman, amewataka walimu na wanafunzi kulitumia ipasavyo chuo hicho kwa kupata mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kujiendeleza kitaaluma, akisisitiza kuwa hilo ndilo lengo kuu la kujengwa kwa jengo hilo
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) Dkt. Shaban Mwichum Suleiman, amesema awali chuo hicho kilikuwa kikitumia gharama kubwa kukodi maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma, hali iliyosababisha haja ya kujenga jengo lao wenyewe litakalokidhi mahitaji ya utoaji wa mafunzo kwa ufanisi zaidi.

.jpeg)
No comments