MATUKIO YA KIHALIFU YAENDELEA KUDHIBITIWA ZANZIBAR.
Na Siti Ali.
Kamisha wa Polisi Zanzibar, CP Kombo Khamis Kombo, amesema matukio ya kihalifu Zanzibar yameendelea kudhibitiwa na kupungua kwa asilimia 24.1% kwa kipindi cha Januari hadi Disemba 2025 ikilinganishwa na kipindi kama hicho 2024.
Kamishna Kombo, ameeleza hayo leo tarehe 23 Januari 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya tathmini ya hali ya usalama Zanzibar, ambapo amesema hali ya usalama imeendelea kuimarika kutokana na juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi.
Hata hivyo, amebainisha kuwa, makosa ya mauaji yamepungua kwa mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka 2024 "Makosa ya mauaji yanatokana na wananchi kujichukulia sheria mikononi kwa tuhuma za wizi ambapo asilimia 94 waliuawa kwa tuhuma hizo, asilimia 04 mauaji yalitokana na wivu wa kimapenzi na asilimia 2 yalitokana na ugomvi kwenye vilabu vya pombe" alisema
Alisema makosa ya kubaka yamepungua kwa asilimia 20.7 kwa mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka 2024. Aidha, katika juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi kuzuia uhalifu, kwa kipindi cha mwaka 2025 kesi 531 zilifanikiwa mahakamani na kuwatia hatiani watuhumiwa.
Hivyo, amewaomba wananchi kuendelea kudumisha ushirikiano na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha kwamba, wanatoa taarifa za wahalifu pamoja na kutoa ushahidi mahakamani.
Amesema, hakuna mtuhumiwa atatiwa hatiani mahakamani bila kutoa ushahidi hivyo jamii inaowajibu wa kufika mahakamani na kutoa ushahidi utakaowatia hatiani watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya kihalifu.
Katika hatua nyingine Kamishna Kombo, amesema jumla ya makosa ya usalama barabarani 71,495 yamekamatwa kwa kipindi cha Januari hadi Disemba 2025 ikilinganishwa na kipindi kama hicho 2024 ambapo yalikamatwa makosa 50,016 na kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa madereva wasiotii sheria za Usalama barabarani.
Kamisha Kombo amewapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa utulivu wao walioonesha katika kipindi chote cha mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025 huku akisisitiza kwamba "Usalama ni Jukumu Letu Sote"


.jpeg)
No comments