TAMWA ZNZ na Wadau Wazindua Tuzo Maalum ya Uandishi wa Habari za Tabianchi, kuongeza Motisha na Kupaza Sauti za Wanawake Zanzibar.
Na Said Khamis.
Katika juhudi za kuimarisha uandishi wa habari unaozingatia usawa wa kijinsia na mchango wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA ZNZ), kwa kushirikiana na Community Forests Pemba (CFP) na Community Forests International (CFI), kimezindua rasmi Tuzo ya “Uandishi wa Habari za Tabianchi za Community Forests.”
Kwa nini Tuzo hizi ni Muhimu?
Wanawake Zanzibar wamekuwa nguzo muhimu katika uhifadhi wa mikoko, kilimo mseto cha agroforestry, na mikakati ya jamii ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, mchango na uongozi wao bado haujaakisiwa ipasavyo katika simulizi za vyombo vya habari.
Utafiti uliofanywa na mradi wa Zanzibar Women’s Leadership in Adaptation (ZanzAdapt) mwezi Juni 2024 unaonesha hali halisi ya changamoto hii. Kati ya habari 4,548 zilizofuatiliwa kutoka vyombo mbalimbali vya habari, ni asilimia 1.1 tu zilizojumuisha sauti za wanawake na wasichana, huku asilimia 0.4 pekee zikionyesha wanawake kama viongozi katika masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Takwimu hizi zinaonesha pengo kubwa la uwasilishaji wa simulizi za wanawake katika vyombo vya habari.
Ni katika muktadha huo ndipo tuzo hizi zimeanzishwa kama jibu la moja kwa moja la changamoto hiyo, na kama jukwaa la kuhamasisha mabadiliko chanya katika uandishi wa habari Zanzibar.
Malengo ya Tuzo
Kupitia Tuzo ya Uandishi wa Habari za Tabianchi za Community Forests, waandaaji wanalenga:
-
Kukuza uandishi wa habari unaoonesha uongozi wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
-
Kutambua na kuthamini waandishi wa habari wanaoandika kwa ubora kuhusu wanawake na masuala ya tabianchi
-
Kuhamasisha uandishi unaozingatia usawa wa kijinsia, ushahidi wa kisayansi na simulizi za mabadiliko chanya kutoka ngazi ya jamii
-
Kuongeza uelewa wa jamii kuhusu nafasi na uongozi wa wanawake katika masuala ya tabianchi Zanzibar
-
Kuweka mazingira ya ushindani chanya kwa waandishi wa habari kuzalisha kazi zenye athari kwa jamii
Aina za Kazi Zitakazoshindanishwa
Tuzo zitahusisha kazi kutoka vyombo vya habari vinne (4), ambavyo ni:
-
Makala maalum kwenye magazeti
-
Vipindi vya redio
-
Vipindi vya televisheni
-
Makala katika mitandao ya kijamii
Kazi zote lazima ziangazie mabadiliko ya tabianchi Zanzibar, kwa kuonesha wazi ushiriki, sauti na uongozi wa wanawake wa Kizanzibari.
Tuzo Maalum
Mbali na tuzo za kawaida, kutakuwepo pia na tuzo maalum nne zitakazotolewa, zikiwemo:
-
Tuzo kwa chombo cha habari kilichoonesha uwajibikaji mkubwa zaidi katika kuandika masuala ya wanawake na tabianchi
-
Tuzo ya mwandishi wa habari kijana (miaka 18–30) katika masuala ya tabianchi
-
Tuzo ya uandishi bora wa habari za tabianchi katika mitandao ya kijamii
-
Tuzo kwa habari iliyoangazia kwa kina nafasi ya wanawake na uongozi wao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Dirisha la Uwasilishaji wa Kazi
Dirisha la kupokea kazi limefunguliwa rasmi kuanzia tarehe 23 Januari hadi 14 Februari 2026, kwa muda wa siku 21. Waandishi wa habari kutoka Unguja na Pemba wanatakiwa kuwasilisha kazi mbili (2) zilizochapishwa au kurushwa hewani kati ya 01 Juni 2024 hadi 31 Disemba 2025.
Kazi zinaweza kuwasilishwa kupitia viungo (links) vitakavyotolewa kwenye mitandao ya kijamii au kuletwa moja kwa moja katika ofisi za TAMWA ZNZ zilizopo Tunguu – Unguja na Mkanjuni – Chake Chake, Pemba.
Kuelekea Hafla ya Tuzo
Hafla ya utoaji wa tuzo inatarajiwa kufanyika tarehe 28 Machi 2026, kuanzia saa moja usiku, na itawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari, taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa kimataifa pamoja na wanajamii.
.jpeg)


No comments