MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIASHARA ZANZIBAR, FURSA KWA WAFANYA BIASHARA NA WAWEKEZAJI.
Na Said Khamis.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na dhamira yake ya kujenga na kuimarisha miundombinu ya kisasa kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuwawezesha kutumia kikamilifu fursa za biashara zilizopo.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, wakati akifungua Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar yanayofanyika katika Viwanja vya Maonesho Dimani, Wilaya ya Magharibi “B”, Unguja.
Amesema maonesho hayo yameendelea kuwa nguzo muhimu inayounganisha sekta ya biashara na huduma, ikiwemo taasisi za serikali na binafsi, makampuni, wajasiriamali, wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na wazalishaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Mhe. Hemed amebainisha kuwa majukwaa ya kibiashara kama hayo ni fursa adhimu ya kukuza na kuendeleza biashara kupitia kujifunza mbinu mbalimbali za kibiashara, kuimarisha ubora wa bidhaa pamoja na kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa.
Aidha, amesema Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kupitia maonesho hayo imeendelea kuweka wazi fursa za uwekezaji katika biashara na viwanda kwa kuimarisha vituo vya uwekezaji katika sekta za utalii, biashara, viwanda, kilimo, uchumi wa buluu pamoja na sekta nyengine zinazochangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hata hivyo, ametoa wito kwa washiriki wa maonesho hayo kuzitumia vyema programu, semina na mijadala iliyoandaliwa kwa lengo la kujifunza mbinu za kufikia masoko ya kimkakati ya kikanda na kimataifa, sambamba na matumizi ya biashara mtandao na sera rafiki za biashara.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha maonesho hayo yanaendelea kupewa hadhi ya kimataifa ili yakidhi vigezo vyote vya matamasha na maonesho ya biashara ya kimataifa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dkt. Habiba Hassan Omar, amesema lengo kuu la kufanyika kwa maonesho hayo ni kukuza biashara pamoja na kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaopata fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zao kitaifa na kimataifa.

.jpeg)

No comments