SERIKALI INATARAJIA KUJENGA SKULI 1,000 KUIMARISHA SEKTA YA ELIMU."SPIKA ZUNGU"
NA SAID KHAMIS.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kujenga skuli 1,000 kwa lengo la kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Mhe. Zungu ameyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa dakhalia za wanafunzi pamoja na nyumba za walimu katika eneo la Kiwani, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Akitoa taarifa ya ujenzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdalla Said, amesema ujenzi wa mradi huo ulianza Septemba 2024 na kukamilika Disemba 2025 kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5. Amesema dakhalia hizo zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 552 pamoja na ujenzi wa nyumba mbili za walimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu Zanzibar, Mhe. Khadija Salim Ali, amesema wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote ya serikali sambamba na kuendeleza ujenzi wa skuli na dakhalia ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid, amesema mkoa huo umeendelea kufanya vizuri kielimu ambapo ufaulu wa mitihani ya Kidato cha Sita (A-Level) umefikia asilimia 100, huku mitihani ya Kidato cha Nne (O-Level) ikipata ufaulu wa asilimia 89.9.
Kutokana na mafanikio hayo, amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa juhudi zake katika kuboresha sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa skuli za ghorofa saba, skuli ya mahitaji maalum, pamoja na mpango wa kujenga skuli tisa mpya za ghorofa katika mwaka wa fedha 2025/2026.

.jpeg)

No comments