Breaking News

ZOEZI LA KUVUNJA NYUMBA BARABARA YA MICHEWENI–SHUMBA LAANZA RASMI



 Nam Mwandishi wetu.

Zoezi la kubomioa nyumba zilizolipwa fidia katika Barabara ya Micheweni–Shumba kisiwani Pemba limeanza rasmi, likiwa na lengo la kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ujenzi wa miundombinu, ikiwemo upitishaji wa mitaro ya maji na kuhakikisha usalama wa wakazi pamoja na watumiaji wa barabara hiyo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, msimamizi wa shughuli hizo kwa niaba ya Afisa Mdhamini wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Ibrahim Saleh Juma, ambaye pia ni Afisa Mwandamizi wa wizara hiyo, Hamad Mfaki Yussuf, alisema kuwa zaidi ya nyumba 20 za wananchi zilizo kwenye mpango wa ujenzi zimeishalipwa fidia kwa mujibu wa tathmini.

Hamad Mfaki Yussuf alifafanua kuwa utekelezaji wa zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa bila vikwazo, sambamba na kuondoa hatari zinazoweza kujitokeza kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya ujenzi.

Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Shumba Mjini, Rahila Ramadhan Juma, alisema kuwa nyumba zote zilizobomolewa tayari zililipwa fidia, na kuwaeleza wananchi kuwa serikali imefuata utaratibu wote wa kisheria kabla ya kuanza kwa uvunjaji huo.



Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Hamad Abdi Saleh, aliwahimiza wananchi wa maeneo hayo kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ile ya barabara inayolenga kuinua hali ya kiuchumi na kijamii.

Baadhi ya wananchi waliolipwa fidia, wakizungumza katika mahojiano na IKHUAN MEDIA, walisema kuwa ni muhimu wananchi kufuata taratibu baada ya kulipwa fidia ili kuepusha kuchelewesha miradi ya maendeleo ambayo ina manufaa makubwa kwa jamii nzima.



Wananchi hao walibainisha kuwa kuchelewesha kupisha miradi ya maendeleo kunaathiri upatikanaji wa huduma muhimu, hivyo ni vyema jamii ikawa mstari wa mbele kushirikiana na mamlaka husika katika utekelezaji wa mipango ya ujenzi wa miundombinu.

Zoezi hilo linatarajiwa kuendelea katika maeneo yote ambayo yanapitiwa na miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo upanuzi wa barabara na uwanja wa ndege kisiwani Pemba, pamoja na maeneo yote ambayo wananchi wamejenga ndani ya hifadhi ya barabara kinyume na utaratibu


No comments