SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA MAZURI KUKUZA KISWAHILI.
Na Mwandishi wetu.12 Decemba 2025.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira bora ya kukuza lugha ya kiswahili ili kufikia malengo ya Dira ya maendeleo ya Zanzibar 2050, ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025 - 2030, mpango wa maendeleo wa Zanzibar 2025/ 2026 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akimuwakilish Mhe. Dkt Hussen Ali MwinyiRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika Ufunguzi wa Kongamano la Tisa (9) la kiswahili la Kimataifa hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Amesema kuwa katika kipindi hichi cha mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambapo teknologia inaongoza katika ufatiliaji wa maarifa ni muhimu lugha ya kiswahili iwe katika mifumo ya kidijitali, tafsiri za kiotomatiki, mitandao ya kijamii, program jalizi na utafiti wa kisayansi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali imedhamiria kukuza lugha ya kiswahili kwa kushirikiana na taasisi binafsi kufanya mashindano mbali mbali ya kiswahili, makongamano na matamasha ya kiswahili kama vivutio vya utalii wa kiutamaduni utakaoifanya Zanzibar kuwa kitovu cha kiswahili duniani.
Aidha, katika kufikia malengo ya Serikali Mhe. Hemed ameiagiza Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kujikita katika kufanya ubunifu kwa kushirikiana na mabaraza ya kiswahili, taasisi za elimu, mashirika ya Kimataifa jumuiya za wataalamu wa lugha, wasanii, vyombo vya habari pamoja na wadau mbali mbali wa lugha ya kiswahili, ili kuhakikisha malengo ya kukuza lugha ya kiswahili yanafanikiwa.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka washiriki wa Kongamano hilo kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza lugha ya kiswahili popote walipo kwa kuziimiza familia zao, wanafunzi wa vyuo na skuli pamoja na jumuiya za Serikali na binafsi kujua thamani ya kiswahili kuwa rasilimali ya maendeleo ya Zanzibar.
Nae Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Riziki Pembe Juma amesema kufanyika kwa makongamano ya Kiswahili yanaunda jukwaa la Kitaifa na Kimataifa la kuchochea mijadala, kutengeneza Sera na kuibua mwelekeo mpya wa ukuzaji wa lugha ya Kiswahili.
Waziri Pembe amesema kufanyika kwa kongamano hilo kunaakisi ukubwa wa nafasi ya kiswahili katika zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia, ufunguaji wa masoko , ujenzi wa jamii zenye maarifa na kupanuka kwa diplomasia ya Kimataifa.
Amefahamisha kuwa matarajio ya Kongamano hilo kupitia mijadala ya kitaaluma itakayofanyika itatoa mapendekezo yatakayoisaidia serikali na taasisi zake kuimarisha sera, mbinu na mikakati ya kukuza kiswahili katika elimu, mawasiliano, biashara na nyanja za kimataifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la kiswahili Zanzibar ( BAKIZA ) Dkt. Saade Said Mbarouk amesema kuwa kongamano la Tisa la kiswahili limekuwa ni daraja la kuwakutanisha wataalamu mbali mbali kutoka duniani na watunga Sera ambao watawasilisha tafiti na mikakati ya kuimarisha kiswahili katika nyanja za elimu , Sayansi teknolojia na maendeleo endelevu.
Amesema kuwa baraza la kiswahili Zanzibari limepata mafanikio makubwa ikiwemo kuanzishwa kwa jarida maalumu la kongamano jarida ambalo linalenga kukuza utafiti, ubunifu na mawasiliano miongoni mwa wataalamu wa kiswahili.
Dkt. Saade amesema jukwaa hilo linaandika historia mpya iliyobeba sauti ya vijana na watafiti chipukizi wanaotaka kuona kiswahili kikipenya katika sayansi, technologia , uchumi na utamaduni wa kidunia




No comments