Breaking News

DKT. MZURI APONGEZA OCGS, ATOA WITO WA MATUMIZI SAHIHI YA TAKWIMU ZANZIBAR



Na Fatma Rajab.

Kongamano la takwimu lililofanyika katika ukumbi wa Michenzani Mall limetoa taswira mpya kuhusu umuhimu wa takwimu katika maendeleo ya Zanzibar, likileta pamoja wadau kutoka taasisi za serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na vyuo vikuu. Kauli mbiu ya kongamano hilo ilikuwa “Kutumia ubunifu wa taarifa na takwimu katika kukuza jamii yenye haki, amani, jumuishi na ustawi kwa Waafrika.”

Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa, ambaye alikuwa mzungumzaji mkuu , alitumia jukwaa hilo kupongeza Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) kwa kazi kubwa na ya uwazi inayofanyika katika kuzalisha na kusambaza takwimu muhimu kwa umma.

Akizungumza mbele ya wataalamu wa takwimu na wadau wa maendeleo, Dkt. Mzuri alisema OCGS imebadilisha mtazamo wa jamii kuhusu takwimu kwa kubadilisha mazungumzo kutoka “tunadhani” kwenda “tunajua,” jambo ambalo limeongeza uwajibikaji na kuimarisha hatua za kisheria na kijamii katika masuala mbalimbali.

Alisisitiza kuwa takwimu sahihi ni msingi wa amani, usawa na haki katika jamii, akibainisha kwamba maamuzi bora hayawezi kujengwa juu ya hisia. Kwa mujibu wa Dkt. Mzuri, mataifa yanayoongozwa kwa takwimu hupiga hatua kwa kasi zaidi kutokana na uamuzi unaotokana na ushahidi.

Katika hotuba yake, aligusia umuhimu wa takwimu katika maeneo nyeti kama uchaguzi, mijadala ya kisiasa, uongozi, pamoja na kuimarisha imani ya wananchi katika mifumo ya serikali. Alibainisha kuwa takwimu zinazotolewa kwa uwazi zina uwezo wa kupunguza uvumi na kutuliza jamii wakati wa mijadala yenye msisimko.


Dkt. Mzuri pia alitaja mafanikio ya ushirikiano kati ya OCGS na wadau kama TAMWA–ZNZ, hasa katika kupata takwimu sahihi za ukatili wa kijinsia. Alisema takwimu hizo zimekuwa msingi wa kampeni, tafiti na utetezi unaolenga kuboresha maisha ya wanawake, watoto na vijana.

Aliongeza kuwa OCGS imepiga hatua kubwa katika kuboresha sensa, tafiti za kaya, takwimu za uchumi, mifumo ya kidigitali na upatikanaji wa taarifa, hatua ambazo zinaweka Zanzibar katika nafasi bora ya kufanya maamuzi ya muda mrefu yenye tija kwa wananchi.

Kuhusu usawa wa kijinsia, alieleza kuwa ongezeko la takwimu za jinsia limechangia kuweka wazi uwiano wa wanawake na wanaume katika uongozi, ikisaidia nchi kupima maendeleo kuelekea malengo ya 50/50 katika nafasi za maamuzi.

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, alitaja changamoto kadhaa zinazohitaji kuzingatiwa ikiwemo kiwango kidogo cha kuripoti matukio ya GBV, upungufu wa data kuhusu ushiriki wa kisiasa, pengo la takwimu za ajira, upatikanaji wa huduma za kijamii na takwimu za ugawaji wa pato katika jamii.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Mzuri Issa alitoa wito mahsusi kwa wadau wote kuongeza kasi ya ushirikiano katika matumizi ya takwimu ili kuimarisha ukuaji wa Zanzibar yenye haki na uwazi. Alisisitiza kuwa OCGS, mashirika ya kiraia, vyuo vikuu, sekta binafsi na vyombo vya habari vinapaswa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha taarifa zinazochapishwa zinatumika kikamilifu kwenye upangaji wa sera, tafiti, utetezi na mijadala ya kitaifa. 


Aliongeza kuwa changamoto kubwa iliyopo ni tabia ya watumiaji wa taarifa kutegemea majibu ya haraka kutoka kwa Afisi ya Mtakwimu Mkuu badala ya kujenga mazoea ya kusoma ripoti, machapisho na takwimu zilizopo wazi mtandaoni. Kwa mujibu wake, uwezo wa Zanzibar kufanya maamuzi sahihi unategemea matumizi ya takwimu na si kuzihifadhi, hivyo wadau wanapaswa kuona takwimu kama rasilimali ya pamoja yenye mchango mkubwa katika kuleta maendeleo na kuimarisha imani ya wananchi katika mifumo ya kitaifa.

No comments