MAKAMU WA PILI WA RAIS AHIMIZA UWELEDI NA MABORESHO SEKTA YA AFYA ZANZIBAR
Na Said Khamis.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewahimiza watendaji wakuu wa wizara ya afya kufanya kazi kwa uweledi ili kuleta mageuzi katika sekta ya afya,
Ameyasema hayo katika kikao kazi kilicholenga kutoa miongozo ya kuboresha utendaji kazi kwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na kutoa huduma bora za Afya kwa wananchi kilichofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Amesema kufanya kazi kwa uweledi kutafanikisha kuleta mageuzi ya kiutendaji katika sekta ya afya kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika hospitali na vituo vya afya kama ilivyoahidiwa na Serikali ya Awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Mwinyi.
Aidha, ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya kuzisimamia Kampuni zilizopewa dhamana ya kutoa huduma katika hospitali za Umma ili kujiridhisha na utowaji wa huduma sambamba na kuangalia ubora wa vifaa tiba, mashine na kuhakikisha upatikanaji wa dawa katika hospitali na vituo vya afya.
Amesisitiza kukaguliwa kwa umakini leseni zote za madaktari kwa kuzingatia viwango vya elimu na vigezo vya uajiri sambamba na kuhakikisha taarifa zote za kiutendaji zinatolewa kwa njia ya mifumo ambayo hurahisisha wananchi kupata huduma kwa wakati.
Sambamba na hayo Mhe, Hemed ameuelekeza Uongozi wa Wizara ya Afya kuzingatia maslahi ya watumishi wakiwemo wataalamu na watumishi wa ngazi za chini kwa kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa wakati ikiwemo malipo ya muda wa ziada, posho za wito na stahiki nyengine.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmed Said amesema suala la nidhamu, uwajibikaji na utayari vimekuwa ni changamoto kubwa katika hospitali na vituo vya afya jambo linalodhorotesha utowaji wa huduma bora kwa wagonjwa na wananchi wanaofuata huduma mbali mbali katika hospitali hizo.
Mhandisi Zena ameeleza kuwa migogoro katika maeneo ya kazi ni adui mkubwa wa kutofikia malengo wanayojipangia hivyo amewataka viongozi wa Wizara ya afya kuacha migogoro baina yao na kujikita zaidi katika kutekeleza majukumu yao kwa uweledi na nidhamu ya hali ya juu ili kufikia malengo ya serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi wa Zanzibar.
Amewataka viongozi hao kutenga muda wa kuzitembelea hospitali na vituo vya afya kuangalia mwenendo nzima wa utowaji huduma kwa madaktari na wauguzi lakini pia kwa kampuni zinazotoa huduma na hospitalini jambo litakalopunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais kwa kuona umuhimu wa kukutana na Uongozi wa Wizara ya Afya na kuwapa maelekezo ambayo yataboresha utendaji wa kazi na utoaji wa huduma bora za Afya nchini.
Dkt. Mngereza ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo na miongozo yote waliyopatiwa na kusema kuwa wamejipanga kuleta mabadiliko makubwa katika kutoa huduma bora za afya kuanzia ngazi ya jamii hadi hospitali za Mkoa .



No comments