Breaking News

WAZIRI LELA ATOA WITO KWA WANAFUNZI KUIMARISHA UJUZI WA TEKNOLOJIA WAKATI

 Na Said Khamis

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema elimu ya matumizi ya vifaa vya teknolojia ni swala la lazima hivyo amewataka Wanafunzi kuongeza juhudi katika kujifunza matumizi ya vifaa hivyo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi laptop kwa Wanafunzi wa Jimbo la gando wanaosoma vyuo vikuu hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Abdulwakil Kizimbani Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.


Amesema Serikali inafanya jitihada kubwa kujenga miundombinu na kuweka vifaa mbali mbali vikiwemo vya (TEHAMA) kwa ajili ya kuwawezesha Wanafunzi waweze kukabiliana na matumizi ya Teknolojia.

Amempongeza Mbunge wa Jimbo la Gando kwa kuunga mkono jitihada hizo za Serikali kwa kutoa laptop 150 kwa Wanafunzi wanaosoma Vyuo vikuu ambao wanatokea jimbo la Gando.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Gando Salim Mussa Omar amesema ameamua kuwapatia Wanafunzi Laptop hizo ili waweze kusoma kwa mafanikio.

Aidha amewataka wazazi kudumisha mashirikiano kati yao na Walimu ili Wanafunzi waweze kufaulu.

Awali Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwalimu Mohamed Nassor Salim amewataka Wazazi kuwapeleka watoto waliofikia umri wa kuandikishwa ili Waweze kuandikishwa kwa mwaka wa masomo 2026.

Amesema zoezi hilo ambalo linafanywa bila malipo yoyote linatakiwa kufanyika katika mwezi huu wa Desemba ili kupata takwimu sahihi za Wanafunzi.

Aidha Mwalimu Mohamed amesema Jimbo la Gando limebarikiwa maeneo mengi Tengefu hivyo Wizara ya Elimu itapeleka Skuli za Msingi na za Sekondari katika maeneo hayo.


No comments