Yanga yatambia kikosi kipana
DAR ES SALAAM; KLABU ya Yanga imesema inajivunia kuwa na kikosi kipana kinachowawezesha kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe alisema wana kikosi kipana kinachoweza kukabiliana na ratiba ngumu ya mashindano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kamwe alisema kwa sasa klabu hiyo inamkosa beki wake mahiri Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ anayetumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitano lakini pia kipa wao Djigui Diarra aliyeumia kwenye mchezo dhidi ya JS Kabylie ya Algeria.
Alisema pamoja na kuwakosa wachezaji hao muhimu kwenye kikosi chao, uwepo wa Frank Assinki na kipa Abutwalib Mshery umeweza kuisaidia timu hiyo kuziba mapengo hayo na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate kwenye mchezo uliopita.
“Sisi hatuna kauka nikuvae, tuna kikosi kipana kinachoweza kukabiliana na changamoto za majeraha na adhabu zinazotokana na mechi mbalimbali tunazocheza.
Umeona hapa tumemkosa Bacca lakini Assinki akaziba pengo lake vizuri, tumemkosa Diarra lakini Mshery ameweza kusimama langoni vizuri,” alisema Kamwe. Kamwe alisema msimu huu kama ilivyokuwa kwa misimu mingine hakuna tofauti na kwamba wataendekea kukusanya mataji yao.
No comments