Breaking News

''TUENDELEE KUKITANGAZAZA KISWAHILI'' DC JUMA



Na mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Unguja Mhea Juma Sururu Juma amelitaka Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kuendelea kusimamia lugha ya Kiswahili ili iendelee kuenea duniani kote.

Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Skuli ya Bumbwini Wilaya ya Kaskazini B' wakati wa kufunga Kongamano la Tisa la Kiswahili la Kimataifa.

Amesema kuwa Baraza la Kiswahili ni chombo kikubwa hivyo ni vyema kuendelea kukitunza na kukisimamia kwa maslahi ya Taifa na jamii kwa uijumla.

Aidha amefahamisha kuwa Zanzibar ni kituo cha Kiswahili Afrika Mashariki, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha anakitumia kwa ufasaha.

Hata hivyo amewashauri washiriki wa kongamano hilo kuyafanyia kazi yale yote yaliyotolewa katika mada na maazimio ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Akitoa maazimio ya kongamano kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) , Mhadhiri Msaidizi kutoka SUZA Dkt. Ziada Tajo Ameir ameishauri Serikali kutumia Kiswahili maskulini katika ngazi zote kama lugha ya Taifa.

Aidha amesema kuwa watumiaji wa Kiswahili wasisahau kujifunza lugha nyengine kwani itasaidia kupata maneno zaidi.

Pia, ameshauri Baraza la kiswahili la Zanzibar na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kufuatilia vyombo vya habari ili kuitumia lugha hiyo kwa ufasaha pamoja na kutoa mafunzo.

Ameongeza kuwa uwenezwaji wa Kiswahili uende sambamba na elimu pamoja na kuongeza jitihada katika kuingiza mtandaoni.

Katika hatua nyengine Dkt. Ziada amesema kuwa Kiswahili kinazidi kutumika nje ya Tanzania hivyo kiendelee kutunzwa kutokana na mabadiliko.

Katika ghafla hiyo Katibu wa Baraza la Kiswahili Dkt Mwanahija Ali Juma amekabidhi vyeti vya ushiriki wa Kongamano hilo.

Ufungaji wa Kongamano la Tisa la Kiswahili la Kimataifa limeambatana na ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria ikiwemo Kisima cha Chini kwa Chini Mangapwani, Kaburi la Rais wa awamu ya pili Marehemu Ali Hassan Mwinyi pamoja na Maeneo ya Makumbusho Fukuchani .


No comments